Hiyo ni kauli ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania MHE. Majaliwa Kassim Majaliwa aliyoitoa leo katika ufunguzi wa
Soko na Ghala la kuhifadhia mazao lililojengwa kwa ufadhili wa kitengo kilichopo katika Ofisi ya Waziri mkuu kijulikanacho kwa jina
la MIVARF, Soko na Ghala vimejengwa katika kata ya Bulige ambapo ni maarufu kwa ulimaji wa zao Mpunga ambapo zaidi ya asilimia ya 60 ya
Mpunga unaopatikana kanda ya ziwa huzalishwa maeneo haya. MHE. Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa Bulige na maeneo yanayoizunguka
kuanzisha Ushirika kama wanavyofanya wananchi wa Lindi na Mtwara ili kuweza kupata bei nzuri za mazao yao kwani mazao huuzwa kwa ushindani
na hivyo kumwezesha mkulima kuuza kwa bei nzuri, MHE. Waziri Mkuu amemtaka Mkuu wa idara ya Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji kusimamia hili
kwa kuhakikisha anawaunganisha wakulima na kuwawezesha kuhifadhi mazao yao sambamba na kuwakutanisha na wanunuzi wa mazao hayo.
Suala la huduma za Afya nalo halikuachwa nyuma kwani ili kuweza kufikia Uchumi wa kati wa nchi yetu ni lazima afya za wananchi wetu ziwe nzuri
hivyo Serikali ya awamu ya tano imejiongeza bajeti ya ununuzi wa madawa na vifaa tiba na hivyo mwananchi aendapo zahanati ahakikishe anapewa dawa
na si kuonyeshwa duka la dawa lililopo karibu na zahanati. Pia MHE. Kassim Majaliwa aliwataka wanabulige kujiunga na Mfuko wa bima ya Afya ya Jamii
wanaoupenda kwani magonjwa hayana taarifa yanapokuja, yaweza kuja wakati huna pesa na hivyo ukalazimika kuuza mifugo au mazao kwa bei ya hasara hivyo
kateni bima ili ziwasaidie, amezitaja baadhi ya bima hizo kuwa ni Bima ya Afya ya Jamii (CHF iliyoboreshwa) ambapo mwananchi atatibiwa ndani ya Mkoa
wake ambapo mwananchi atachangia Tsh. 30000 kwa mwaka na atapatiwa huduma yeye na wategemezi wengine 5 mwaka mzima bure. Pia kuna bima ya ushirika
ambapo mwanachama huchangia Tsh. 76000 kwa mwaka na hutibiwa sehemu yeyote Tanzania katika Hospitali za Serikali, hii inahusisha pia matibabu katika
Hospitali za Rufaa kama KCMC, MBEYA, MUHIMBILI.
Waziri Mkuu ameahidi kutoa pesa tena ili kuongeza Ghala katika sehemu nyingine ya Halmashauri ya Msalala sambamba na kuleta gari la kubebea wagonjwa
(Ambulance), MHE. Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa Halmashauri kupitia Mkurugenzi mtendaji, Mwenyekiti wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Baraza zima
la Madiwani kwa uamuzi wa kuruhusu wafanyabiashara kufanya biashara katika eneo hilo bure kwa muda wa Miezi 6.
Nae Mbunge wa Jimbo la Msalala ameshukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa Soko na Ghala ambavyo kwa sasa vinatumika, huu ni ukombozi kwa wananchi wa
Bulige. Jambo ambalo wanabulige wanaiomba Serikali ni kuwezesha wananchi wa Bulige na jimbo la Solwa kuanzisha kilimo cha umwagiliziaji kwani maeneo haya
yana mbuga nzuri inayofaa kwa kilimo muda wote. Pia pana changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama licha ya kuwepo mradi wa maji ya ziwa Viktoria
kwani mabomba yamekuwa yakipasuka mara kwa mara na mwisho amebainisha ubovu wa barabara zinazotumika ndani na nje ya Msalala na ameomba Serikali kutatua
changamoto hizo sambamba na kuwaalika wawekezaji kuleta mashine za kukoboa Mchele kwani miundombinu yote muhimu ya uanzishaji viwanda hivyo vipo na
Halmashauri ipo tayari kutoa maeneo ya ujenzi wa viwanda hivyo bure.
Mhe. Waziri Mkuu amehitimisha ziara yake katika Halmashauri ya Msalala kwa kujibu changamoto zilizojitokeza kwa kumtaka mhandisi wa maji afuatane nae mchana
wa leo atakapoondoka kwa ndege kuelekea Dares salaam ili akanunue kifaa cha kupunguza kasi ya maji toka bomba kubwa na hivyo kuwezesha wakazi wa Bulige
kupata maji kwa uhakika. Waziri mkuu amemkaribisha naibu waziri wa ujenzi na miundombinu MHE. Kwandikwa mbunge wa Jimbo la Ushetu ambaye ameeleza jitihada
zinazofanyika kuhakikisha barabara zote zinapitika muda wote ikiwemo barabara ya Kahama Mwanangwa kuwekewa lami hapo baadae, pia NTALULA itaendelea na marekebisho
ya barabara zilizoharibika kwa mvua ili ziweze kutumika.
Na mwishoni amemkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama mpya ndugu. Anamringi Macha kuwasilimia wananchi wa Bulige, ndg. Macha amemshukuru Rais kwa kumteua katika nafasi
hiyo na kuwaomba wananchi wote ndani ya Wilaya ya Kahama kutoa ushirikiano ili kuwezesha malengo yaliyowekwa na Serikali kufikiwa kwa urahisi.
Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Msalala.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.