Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama leo tarehe 31.07.2024 katika kikao chake cha robo ya nne cha kupitia taarifa za shughuli zilizotekelezwa na Halmashauri hiyo katika kipindi cha mwezi mei hadi Juni 30,2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo katika Kata ya Ntobo umbali wa KM.33 kutoka Kahama Mjini. Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bwana JUdica Sumari amesema katika kipindi cha robo ya nne Halmashauri umevuka lengo la ukusanyaji mapato ajenda ambayo ni kipaumbele kwa ustawi wa Halmashauri na kuwaomba waheshimiwa Madiwani wote waendelee kuunga mkono kwa vitendo ili kuhakikisha mianya yote ya utoroshaji wa mapato ya Serikali inadhibitiwa.
Kikao hicho ilikuwa ni mwendelezo kwani Baraza hilo hufanyika kwa muda wa siku 2 ambapo katika siku ya kwanza,baraza hupokea taarifa za shughuli zilizotekelezwa ngazi ya kata ikiwemo kupeana uzoefu wa utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika taarifa zao. Kwa ujumla shughuli nyingi za ujenzi na ustawi wa jamii ya Watanzania zimefanyika ikiwemo usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo inayopewa fedha kutoka mfuko mkuu wa Serikali, mfuko wa jimbo na mapato ya ndani ya Halmashauri.Baraza limepongeza Serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais DR.Samia Hasain Suluhu kwa kufanikisha miradi mingi ndani ya Halmashauri ya Msalala.
Siku ya pili ya kikao Baraza limepitia Taarifa za utekelezaji za kamati za Uchumi,Ujenzi na Mazingira ambapo baraza limeomba miundombinu hasa ya barabara na umeme vijijini viimalishwe kwani tunaelekea kipindi cha masika hivyo wakandarasi wasipofanya kazi zao katika kipindi hiki, ni dhahiri kazi hazitafanyika tena na hali ya barabara zetu itakuwa mbaya sana kwani Halmashauri hii 75% ya eneo lake ni mbuga. Suala hili litafanyiwa kazi na TARURA iliyowakilishwa na Injinia Butondo ambaye ameomba Halmashauri kushirikiana na TARURA kwani maeneo mengi yameathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha na fedha iliyopo ni ndogo ukilinganisha na mahitaji.
Katika uwasilishaji wa Taarifa ya Kamati ya Elimu,Afya na maji, mwenyekiti wa kamati hiyo MHE.Joseph Manyara Diwani wa kata ya Segese amemshukuru Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kuwezesha miundombinu mizuri kwenye shule na ametaja baadhi ya miundombinu hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa ya kisasa yakiwa na thamani zake na kuwaomba wananchi wote na hasa wanaozunguka maeneo ya shule kuvitunza ili kuunga mkono maendeleo yanayofanywa na Rais wetu. Nitoe pongezi kwa idara ya Elimu sekondari inayoongozwa na Mbobezi wa Hisabati NDG.Seleka ntobi,mdhibiti ubora wa elimu Msalala bwana Raphael Ikombe kwa usimamizi mzuri. Kipekee niwapongeze walimu wote ndani ya Halmashauri yetu kwa kuwezesha wanafunzi kufaulu vizuri masomo yao. Sisi kama Halmashauri tulishajipangia kutoa zawadi kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri ambapo tunatoa Tsh. 7000 kwa kila somo kwa ufaulu wa daraja A, na Tsh. 4000 kwa daraja B.
Akiwasilisha Taarifa ya ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya kidato cha pili na nne, Afisa Taaluma Sekondari Bwana Elias Nyabenda amesema Jumla ya Tsh.2,080,000 imelipwa kwa wanafunzi wa kike na kiume walioongoza na kupata daraja la kwanza lenye alama 4 mpaka 7 ambapo fedha imetolewa sawa sawa kwa jinsia zote mbili na kufanya hesabu kuwa Tsh.2,080,000. Kwa upande wa kidato cha sita jumla ya Tsh.850,000 imelipwa kwa wanafunzi wasichana 4 wenye ufaulu wa juu na Tsh.1,975,000 imelipwa kwa walimu waliofanikisha ufaulu wa wanafunzi hao. Sambamba na haya,halmashauri imetoa zawadi kwa shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya Taifa kidato cha pili na nne ambapo Tsh.1,280,000 zimelipwa na hivyo kufanya malipo ya fedha Taslimu kuwa Tsh.17,791,000.
Si malipo ya fedha pekee yaliyotolewa kwa shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya kitaifa bali shule hizo pia zimepatiwa vitendea kazi,ambapo shule za Mega mshindi wa kwanza matokeo ya kidato cha pili mwaka 2023 amejipatia photokopi mashine,Ngaya sekondari mshindi wa kwanza matokeo ya kidato cha nne 2023 amejipatia photokopi mashine,mshindi wa pili matokeo kidato cha pili na nne ni mwl.nyerere sekondari ambaye amejipatia photokopi mashine 2 na mshindi wa 3 kwa matokeo ya kidato cha pili na nne amejipatia printa 2 vyote kwa pamoja vikiwa na gharama ya Tsh.10,400,000 na hivyo kufanya hesabu kuu ya malipo ya motisha kwa wanafunzi, walimu na shule kuwa Tsh.28,191,000.
Akihitimisha kikao hicho mwenyekiti wa Halmashauri MHE.Mibako Mabubu amepongeza wanafunzi na walimu kwa matokeo mazuri ya mitihani ya kitaifa na kutoa rai kwa wazazi hasa wanaosuasua kuchangia chakula kwa watoto wao kuweza kuchangia ili watoto hao waweze kupata chakula shuleni kwani ufaulu huchangiwa pia kwa wanafunzi kujifunza wakiwa wameshiba sambamba na kuwa na mazingira mazuri ya kujifunza wakiwa nyumbani.Halmashauri tuliona ni vema tuanze kutoa zawadi kwa wanafunzi, walimu na shule ili kuboresha na kuamsha hali za kujifunza na takwimu zinaonyesha baada ya kufanya hivi matokeo mazuri yanapatikana kila mwaka,jamii yote ya wakazi wa Halmashauri ya Msalala tufurahie mafanikio haya.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.