Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Msalala limepitisha bajeti ya Halmashauri ya Msalala yenye thamani ya Tsh: Bilioni 2.1 huku vipaumbele vya bajeti hiyo vikiwa vimewekwa kwenye suala la uwekezaji na ukusanyaji mapato na kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo sambamba na kubuni vyanzo vipya. Halmashauri katika mwaka wa fedha 2019/20 imejipanga kujenga uzio katika minada ya Bulige na Masabi ili kurahisisha zoezi la kukusanya ushuru katika minada hiyo sambamba na kujenga stendi katika kata za Segese, Isaka na Bulige.
Akiwakilisha makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji , Afisa mapato bwana Samwel Seritongwe amesema Halmashauri imeamua kuandaa bajeti yenye uhalisia na hivyo kujiepusha na kuwa na bajeti isiyotekelezeka kwani kwa miaka 2 iliyopita Halmashauri iliandaa bajeti ikiwa na matarajio ya Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu ungeongeza uzalishaji suala ambalo bado mgodi huo haujaongeza uzalishaji huo mpaka sasa. Ni vizuri kuandaa bajeti kutokana na vyanzo tulivyonavyo na endapo kuna fedha itapatikana nje ya bajeti mwongozo wa bajeti unaruhusu ongezeko hilo kuingizwa kwenye bajeti kwa kufanya marekebisho ya bajeti muda wowote.
Wajumbe wa Baraza hilo wakiongozwa na mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mibako Mabubu wameridhia makadirio hayo na kumwomba mkurugenzi Mtendaji na wataalamu wa Halmashauri kuhakikisha vyanzo vyote vya mapato vinasimamiwa kwa ufasaha sambamba na kuomba chanzo cha upimaji ardhi kwa kutumia makampuni katika kata za Segese, Mega, Bugarama, Bulyanhulu, Bulige na Isaka liingizwe ili kuongeza mapato ya Halmashauri, suala ambalo Mkurugenzi Mtendaji (W) amesema lipo kwenye bajeti na hivyo baraza likaomba mambo yote yaliyopitishwa katika bajeti hiyo yatekelezwe kwa vitendo.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtendaji (W) amesema Serikali ilizitaka Halmashauri kuwasilisha maandiko ya miradi ya jamii ili Serikali iweze kuleta fedha za kumalizia miradi viporo zilizopo kwenye maeneo yetu suala ambalo Halmashauri ililipokea na kupeleka maandiko kupitia Mbunge wa jimbo la Msalala na tayari Serikali imeyapokea maandiko hayo na muda wowote kuanzia sasa fedha za miradi ya kijamii itaingizwa na kutumwa kwa ajili ya utekelezaji hivyo Serikali itatekeleza shughuli za miradi ya kijamii kupitia maandiko yaliyowasilishwa TAMISEMI sambamba na kuwapa wadau wetu shughuli ambazo tungependa ( jamii ) itekelezwe kwani shughuli za sasa ni lazima mahitaji yatoke kwa wananchi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
MSALALA
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.