Halmashauri ya Msalala imepanga kutoa fedha zote zinazotakiwa kwenye vikundi vya wanawake ,vijana na walemavu kwa mwaka wa fedha ujao yaani 2020/21 ili kuwezesha makundi hayo kujiendeleza katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo kama Ilani ya chama tawala inavyosema “ kuwezesha wananchi kiuchumi”. Kauli hii imesemwa na mweka Hazina wa Halmashauri hiyo ndugu Masatu Mnyoro wakati wa kikao cha wataalamu cha kujadili taarifa za mwisho wa wiki ambacho hufanyika kila Jumanne ya kila wiki.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii ,jinsia wanawake na watoto ndugu Neema Katengesha amesema kwa mwaka wa fedha halmashauri ya Msalala imefanikiwa kutoa kiasi cha Tsh. Milioni mia mbili arobaini ambapo Milioni mia mbili na ishirini ni fedha zilizotokana na makusanyo ya mapato ya ndani na Milioni ishirini ni fedha za marejesho ya vikundi ambazo Halmashauri iliwakopesha. Afisa maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na watoto huyo ameendelea kusema kuwa Halmashauri inakumbana na changamoto ya wananchi wanaokopa kutokurudisha fedha kwa wakati suala ambalo linasababisha vikundi vingine kutopewa fedha kwa wakati.
Kwa upande wao wajumbe wa kikao hicho wamepongeza jitihada zinazofanywa na Halmashauri hususani kutoa asilimia kumi kwa kila wiki ya makusanyo yake kwa mukundi ya wanawake, walemavu na vijana na kuitaka Halmashauri kuchagua vikundi vichache ambavyo vitafanya mradi mkubwa ambao utawezesha wajasiriamali hao kujitegemea na hivyo kuinua pato la Halmashauri na Taifa kwa ujumla. Sambamba na hili wajumbe wameitaka Halmashauri kuanza kutumia vyombo vya sheria kuhakikisha mikopo inayokopeshwa inarejeshwa kwa wakati ili iweze kuwanufaisha wajasiriamali wengi.
Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano
MSALALA
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.