Kamati ya fedha, uongozi na mipango ya Halmashauri imewataka wamiliki wa mashamba yanayochimbwa madini na wamiliki wa migodi ya wachimbaji wadogo wadogo kuhakikisha makubaliano waliyowekeana na Halmashauri yanatekelezwa na kukamilika kwa wakati ili miradi hiyo ianze kutumika na jamii. Miongoni ya miradi hiyo ni ujenzi wa zahanati katika kitongoji cha kakola namba 9 ili kuwezesha jamii ya maeneo hayo kufaidika kutokana na uwepo wa uchimbaji madini.
Agizo hilo limetolewa leo wakati wa kikao cha kamati hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo ambapo mwenyekiti wa kikao hicho MHE. Mibako mabubu amewataka wataalamu kusimamia maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo. Katika kikao hicho wajumbe mbalimbali wamehudhulia akiwepo mbunge wa jimbo la Msalala MHE. Ezekiel Maige, mwakilishi wa katibu Tawala (M) bwana Kasani, wajumbe wa kamati hiyo na wataalamu wa Halmashauri.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni Halmashauri kuhakikisha mapato yanayokusanywa yanapelekwa benki kwa wakati ili kujiepusha na hoja za ukaguzi ambapo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ndugu Masatu Mnyoro amesema tayari kamati tendaji imeanza kuchukua hatua stahiki kwa wakusanya mapato ambao bado hawajapeleka fedha benki sambamba na hilo wajumbe walitaka watumishi kuwatumikia wananchi kwa moyo mmoja na kujiepusha na kuwanyanyasa wananchi kwani jamii inawategemea sana wataalamu hao.
Nae MHE. Frola Sagasaga diwani wa kata ya Mwalugulu ametaka Halmashauri kuchukua tahadhali kwa kuhakikisha inasimamia ujenzi wa vyoo na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yote yanayojihusisha na uchimbaji dhahabu na hasa katika eneo la namba 9 na namba 2 kwani maeneo hayo hali ya usafi hairidhishi na isitoshe tunaelekea katika msimu wa mvua za masika hivyo hali hiyo ikiachwa iendelee ni dhahili kuwa ugonjwa wa kipindupindu unaweza kutokea na hivyo kuathiri afya za wananchi, suala ambalo limeungwa mkono na wajumbe wote wa kamati hiyo. Akijibu hoja hiyo ndugu Masatu Mnyoro amesema suala hilo lipo katika utekelezaji kwa kuwa tayari mkuu wa Wilaya alishatoa maelekezo na hata hivyo Halmashauri inalichukua kwa utekelezaji.
Akihitimisha kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufanya kazi kwa umoja kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaletewa maendeleo hasa katika kuhakikisha mapato yanakusanywa kwani kila diwani ana wajibu wa kuhakikisha katika kata yake vyanzo vilivyopo anavisimamia na kutoa taarifa Halmashauri ili kuwezesha Halmashauri kujipatia mapato. Ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha soko la dhahabu katika eneo la uzalishaji kwani imekuwa ni chanzo kizuri cha mapato kwa Halmashauri.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya Msalala
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.