Idara ya Afya
Halmashauri ya Msalala ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za Afya 29 kati yao 23 vya serikali ambapo,Vituo vya Afya 3 vya Serikali na 2 vya Binafsi na Zahanati ni 20.
Huduma mbalimbali za afya zikiwemo huduma za chanjo, ushauri nasaha na upimaji wa VVU, na huduma za mama na mtoto, huduma za wagonjwa wa nje(OPD),huduma za kujifungua akina mama,kliniki za Afya ya uzazi na mtoto,huduma za mkoba za chanjo na uzazi wa mpango,huduma za tiba na matunzo kwa WAVIU (CTC) zinatolewa kwenye vituo 8.Halmashauri inatambua umuhimu wa Afya bora kama nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini.
Kwa mantiki hii afya inalenga kuwa na ustawi endelevu kwa jamii, kwa kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa zilizopo katika kuleta maisha bora. Upatikanaji wa afya bora unahitaji uwezeshaji wa jamii iwe na uwezo wa kushiriki, kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kuwaletea maendeleo katika ngazi mbalimbali. Hivyo basi, Huduma za Afya ndani ya Halmashauri zimeendelea kutolewa kwa kiwango cha kuridhisha kutokana na mabadiliko endelevu yanayofanyika katika Sekta ya Afya kwa lengo la kuleta uwiano katika upatikanaji wa huduma bora za Afya Mijini na Vijijini.
Kituo cha afya cha Lunguya ndio kituo pekee kinachotoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa wa dharura wenye matatizo ya uzazi na hadi sasa jumla ya akina mama 67 wamefaidika na huduma hizo.Kituo hiki kimepunguza adha ya wananchi kulazimika kusafirishwa kwenda Hospitali ya Mji wa Kahama kupata huduma hizo. Aidha, vituo 8 vinatoa huduma za tiba na matunzo pamoja na huduma za mikoba za CTC katika vituo 5.Wananchi wa Msalala bado wanakabiliwa na magonjwa makubwa ya kuambukiza ambayo ni UKIMWI, malaria na kifua kikuu. Aidha, afya ya uzazi na mtoto inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga. Vile vile magonjwa yasiyo ya kuambukizwa yameanza kujitokeza kwa wingi kutokana na mabadiliko ya mienendo na tabia ya kuishi.katika kutoa huduma za kinga, mapambano yameelekezwa kutokomeza magonjwa yanayosababisha vifo vya watoto chini ya umri wa mwaka 1 na chini ya miaka 5 na kina mama wajawazito. Katika utoaji huduma hizo msisitizo umewekwa kwenye utoaji chanjo na elimu, Aidha Halmashauri inaendelea na jitihadha za kudhibiti na kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.Halimashauri pia kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya katika ngazi zote. Katika kuboresha utoaji wa huduma, mafunzo mbalimbali yamekuwa yakitolewa kwa watumishi kufuatana na taaluma zao na mahitaji. Vile vile halmashauri imeendelea kutoa huduma kwa makundi maalumu. Aidha, jamii imeendelea kushirikishwa kikamilifu katika kutambua, kupanga na kutekeleza mipango ya afya ikiwemo usafi wa mazingira na usafi wa mtu binafsi.
Halmashauri imeendelea kupambana na janga la UKIMWI na magonjwa mengine ya kuambukiza na yasiyo yakuambukiza, kwa kuanzisha na kutekeleza mikakati maalum na kuelemisha jamii ili kupunguza maambukizi mapya, kujikinga na kuchukua hatua ya matibabu sahihi mapema.
Mafanikio
Halmashauri ya Msalala kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imeendelea kuboresha huduma za Afya za kinga na tiba dhidi ya magonjwa, pia utekelezaji wa mipango na mikakati ya huduma za afya na ustawi wa jamii ambayo imepelekea kuwepo na mafanikio katika maeneo mbalimbali.Ili kuimarisha malengo yaliyokusudiwa katika kuboresha ubora na ufanisi wa utoaji wa huduma za Afya, Idara inafanya kazi katika maeneo makuu sita ambayo ni Utoaji wa huduma, Raslimali Watu, Mfumo wa Taarifa za Afya, Upatikanaji wa Dawa muhimu, Fedha, Uongozi na Utawala bora.
Ongezeko la Upatikanaji wa Huduma za Afya karibu ya wananchi.
Idara inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Afya Msingi (MMAM-2007/17) unaotaka kila Kata kuwa na kituo cha Afya na Kila kijiji kuwa na Zahanati.
Wananchi wameelimishwa juu ya umuhimu wa huduma za Afya na kuhamasishwa kutumia huduma hizo hali ambayo imechochea mahitaji makubwa kwa kila ngazi ya kutolea Huduma Upatikanaji wa huduma za afya kwa karibu kwa wananchi imekuwa ni kipaumbele kwa Idara Hali kadhalika afya kwa wananchi imekuwa ikiboreshwa licha ya kuwepo kwa changamoto zinazojitokeza nyakati mbalimbali.
Idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali imeongezeka kutoka vituo 16(Zahanati 14 na vituo vya afya 2) mwaka 2014 hadi vituo 23(vituo vya afya 3 na Zahanati 20). Aidha, Vituo vya Afya 2(Lunguya na Chela) vimeanzisha huduma za upasuaji kwa kina mama wajawazito wenye matatizo mbalimbali ya uzazi na hadi kufikia Disemba 2016 jumla ya kina mama wajawazito 67 wamefanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya uzazi. Aidha, zahanati mpya nne(Mbizi, Mwanase, Mwakata na Matinje) zinatarajia kufunguliwa mwaka 2017 ili kuimarisha huduma za Afya
Huduma kinga Kama vile utoaji elimu ya Afya kwa wananchi, na usafi wa mazingira zimeendelea kutolewa kwa kiwango kikubwa. Vile vile Kampeni mbalimbali zimefanyika ikiwemo; Kampeni za chanjo-Polio na Surua, Kampeni za utoaji Vitamin A, na dawa za Minyoo zote hizo zinalenga kutokomeza magonjwa. Vifo vya watoto wachanga na vifo vitokanavvyo na uzazi Vimepungua ukilinganisha na mwaka 2014.Hata hivyo, makundi maalum ambayo ni; wazee wasiojiweza, watu wenye ulemavu, watoto wenye umri chini ya miaka 5 na wanawake wajawazito wamekuwa wakipata huduma za Afya bila malipo.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.