TAARIFA FUPI YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA IDARA YA MAJI
Idara ya maji ni mojawapo ya Idara sita (6) za Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Mkoa wa Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ina Jumla ya wananchi 250,727 kulingana na Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012, kati ya Wananchi hao watu 129,376 wanapata huduma ya Maji ambao ni sawa na asilimia 51.6 wanaopata maji safi na salama. Miradi ya maji ya bomba na Visima ipo 347 inayotoa huduma ya maji katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kati ya miradi hiyo visima virefu vipo 48 vilivyofungwa pampu za mkono, visima vifupi vipo 275 vilivyofungwa pampu za mkono, mabwawa 6, miradi 6 ya maji ya Mserereko(Gravity scheme) na miradi miwili inatumia nguvu ya jua Kwa sasa kuna Jumuiya za watumia maji 21, ambapo kati ya hizo 16 zimesajiliwa na 5 zimehamasishwa ziko kwenye mpango wa kusajiliwa.
Halmashauri inategemea kuongeza huduma ya maji safi na salama kutoka 51.6 mpaka 57.08 kupitia miradi ya maji miwili inayokaribia kuanza kujengwa katika vijiji sita vya kata ya Bulyanhulu kupitia mradi wa Ushirikiano kati ya Halmashauri za Wilaya ya Msalala, Nyangh’wale na Shinyanga pamoja na mradi wa maji wa Kagongwa – Isaka ambayo ujenzi wake unategemea kujengwa kuanzia mwezi Januari na mradi wa maji wa Igombe na Mhama uliopo kwenye hatua za mwisho za Ujenzi.
Idara ina watumishi saba (7) kwa ujumla wake ikiongozwa na Mkuu wa Idara na Mafundi Sanifu Sita (06).
Maji ni muhimu kwa viumbe vyote duniani, bila maji hakuna uhai. Aidha maji ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Kiwango cha maendeleo ya jamii yoyote kinategemea kuwepo kwa maji ya kutosha na yenye ubora unaotakiwa. Katika hali yake ya asili, maji ni sehemu ya mazingira ambapo wingi na ubora wake ndio unaosaidia katika kuamua jinsi maji yatakavyotumika. Upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na usafi wa mazingira ni muhimu katika kulinda afya za wananchi. Utumiaji wa maji ambayo sio salama na uhaba wa maji huchangia katika kusababisha milipuko na kuenea kwa magonjwa kama kuhara na kipindupindu. Japokuwa maji ni muhimu kwa uhai wa viumbe, na maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hakuna uwiano wa mgawanyo wa maji ulio sawa kati ya sehemu moja na nyingine na katika majira mbalimbali ya mwaka. Aidha, wingi wa maji yanayofaa kwa matumizi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi una kikomo, na maji hayo pia yanaweza kuathirika kirahisi.
Lengo kubwa la Halmashauri ni kuhakikisha kuwa inatoa huduma bora za maji ili kufikia dira ya maendeleo ya Taifa ya 2025 kuhakikisha kuwa 85% ya Wananchi wote wanaoishi vijijini wanapata huduma ya maji kwa umbali usiozidi mita 400.
Katika utaratibu Halmashauri iliojiwekea inategemea kuanza ujenzi wa mradi Mkubwa wa maji unaotegemea kujengwa kwa ushirikiano na Halmashauri tatu ambazo ni Msalala kama msimamizi mkubwa wa mradi, Halmashauri ya Wilaya ya Nyangh’wale,Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Mgodi wa madini ya Dhahabu wa ACACIA (Bulyanhulu). Mradi huu unategewa kuhudumia vijiji 15 ambapo watu 100,437 watanufaika na huduma ya maji kwa awamu ya pili ya Ujenzi wa mradi huo.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.