Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bi. Rose Robert Manumba ameitaka jamii ya watanzania hasa wa Halmashauri ya Msalala kujenga mazoea ya kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimarisha Afya zao,ushauri huu umetolewa Tarehe 08/09/2024 wakati wa kukabidhi zawadi kwa mshindi wa mashindano ya Mahona Cup ambayo hufanyika kila mwaka kwa kuzishirikisha Timu za mpira wa miguu za Kata za Mega, Segese, Shilela, Lunguya, Bugarama, Bulyanhulu, Chela na Timu moja kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe ambapo kwa mwaka 2024, Timu za Mguu Tageti na Segese namba 3 zote kutoka kata ya Segese zilifanikiwa kucheza fainali.
MKurugenzi Mtendaji huyo amempongeza NDG.Patrick Mahona Mdhamini wa mashindano hayo na wadau wengine waliounga mkono kufanikisha mashindano hayo na akaahidi kutoa ushirikiano
muda wote Taasisi yake itakapohitajika kufanya hivyo kwani michezo huimarisha afya,hukuza mahusiano baina ya rika mbalimbali,huleta ajira na kuimarisha ushirikiano na zaidi ya
hapo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi inasisitiza kukuza na kuibua vipaji kwa vijana wa Kitanzania kupitia michezo hivyo ni jukumu letu kuhakikisha dhana hii inatekelezeka
kwa vitendo.
Akimkaribisha mgeni rasmi wa hafla hiyo,diwani wa Kata ya Segese MHE.Joseph Manyara amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji kwa kukubali kuhudhuria hafla hiyo na kuomba jamii kuendelea
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya 6 kupitia viongozi wa Halmashauri na Kata kwa pamoja ya kuwezesha kuwaunganisha wadau mbalimbali ndani ya kata ya Segese
na kuwezesha mashindano hayo kufanyika kwa ukamilifu na akaomba wananchi kuendelea kukiamini Chama Tawala kwani mambo mazuri yanabuniwa na viongozi wabunifu.
Nae Mdhamini wa Mashindano hayo Bwana Patrick Mahona amewashukuru wadau mbalimbali waliomuunga mkono katika kuhakikisha mashindano haya yanafanikiwa na kuomba wadau zaidi kujitokeza
ili kuwezesha mashindano haya kupanua wingo na kufanyika kihalmashauri kwani zipo faida nyingi kupitia mashindano haya.Amezitaja baadhi ya faida kuwa ni kuwezesha watoto yatima na
wanaoishi katika mazingira magumu kuendelea na masomo kwa kuwalipia gharama zao za masomo ambapo wapo vijana 3 wanaendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.Sambamba na hilo mashindano
hayo yameongeza mori kwa wanafunzi kufanya vizuri kimasomo na kuibua vipaji kwani Shule ya Sekondari ya Mwl.Nyerere imeshiriki mashindano hayo na kuibuka kuwa mshindi wa 3 kati ya Timu 32
zilizoshiriki kwenye mashindano ya Mahona Cup 2024.
Gharama zilizotumika katika maandalizi, zawadi na utekelezaji wa mashindano ya Mahona Cup kwa mwaka 2024 ni Tsh.7,538,000 na washiriki wa mashindano hayo wamewapongeza wananchi wa kata ya Segese
kwa kujitokeza kwa wingi katika kuangalia mashindano hayo na kujitoa kwa hali na mali kuchangia pale ilipobidi,hii inaonyesha umoja na kuhamasika kwa hali ya juu kuunga mkono michezo kwani michezo
ni furaha na wameomba Serikali, wawekezaji na wadau mbalimbali kuwekeza viwanja vya michezo ndani ya kata ya Segese ili kuwezesha kuongeza mapato ya Serikali kwani jamii ya Segese na Kata jirani
zinathamini sana michezo.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.