Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Msalala limeiomba Serikali kuweka kapaumbele kwenye kukamilisha miradi viporo vilivyopo ndani ya Halmashauri hiyo kwani kwa kufanya hivyo itakuwa inaunga mkono jitihada zilizoanzishwa na wananchi kwa kuwa tayari wananchi walishachangia nguvu zao katika ujenzi wa maboma kama sera ya miaka ya nyuma ilivyotaka, maelezo hayo yametolewa muda mfupi na Mhe. Enos Bugondo diwani wa kata ya Jana na kuungwa mkono na Wah. Madiwani wote kwa kusema imekuwa ni kero kwani Halmashauri ina idadi kubwa ya maboma.
Mkurugenzi mtendaji (W) ndugu Simon Berege akijibu hoja hiyo amesema Halmashauri imefanya maandiko na kuyapeleka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo mfano mzuri ni Mgodi wa Accacia ambapo katika robo iliyopita iliweza kutoa mifuko ya simenti 1600 ambayo imegawanywa katika kata mbalimbali ikiwa na lengo la kukamilisha miradi hiyo viporo, amesema kwa sasa Serikali ya awamu ya tano inahimiza wananchi kujenga mradi mzima na Serikali inaleta wataalamu ili mradi uanze kutumika pindi unapokamilika na iwapo Pesa inatolewa hutolewa zikidhamilia kukamilisha ili wananchi waone matunda ya mradi husika hivyo amewaomba waheshimiwa madiwani wawaelimishe wananchi juu ya mabadiliko haya.
Nae mkuu wa idara ya Maji (W) mhandisi marko chogero akijibu hoja kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji (W) amesema Serikali imeridhia kutoa Zaidi ya bilioni 3 katika mwaka wa fedha huu kukamilisha miradi ya maji ya Ngaya nduku Busangi, upanuzi wa mradi wa maji katika kata za Bulyanhulu na Bugarama na marekebisho ya mradi wa maji katika kata ya Segese sambamba na ukarabati wa visima virefu na vifupi vilivyopo ndani ya Halmashauri.
Katika Baraza hilo waheshimiwa Madiwani wameiomba Halmashauri ihakikishe mapato yanakusanywa sambamba na kubuni vyanzo vipya vya mapato kwani mapato yameshuka sana kutokana na mgodi kusimamisha shughuli zake za uzalishaji kutokana na agizo la Serikali hivyo Halmashauri ihakikishe gari iliyotengwa kwa shughuli za mapato litumike kwa shughuli hiyo pekee suala ambalo limekubaliwa na uongozi wa Halmashauri hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Msalala
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.