Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala limeipongeza Timu ya Wataalamu inayoongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw.Charles Fussi kwa kuandaa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 vizuri huku vipaumbele vya Halmashauri ikiwa ni kuondoa utegemezi wa mapato ya ndani kutoka mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu na kuwezesha Halmashauri kujitegemea kwa mapato yake pekee.
Akiwasilisha Mpango wa bajeti hiyo Mweka Hazina bw. Masatu Mnyoro amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Halmashauri imejipanga kuondoa tozo sumbufu kwa wananchi sambamba na ununuzi wa maeneo katika kata za Bulyanhulu, Isaka na Segese kwa ajili ya uwekezaji.Pia katika mwaka huo Halmashauri imepanga kuboresha stendi zake kwa kuongeza vibanda ndani ya stendi hizo.
Bajeti iliyopitishwa na Baraza hilo ni Tsh.bilioni 4 na milioni mia moja na ishirini tu ( 4,120,000,000) kutoka chanzo cha mapato ya ndani huku vipaumbele vikiwa ni ujenzi wa uzio minadani, umaliziaji wa kituo cha maegesho ya malori Isaka na baadae Segese na uhamasishaji wa mazao mbadala ndani ya Halmashauri.
Akifunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Mibako Mabubu amesema Halmashauri ihakikishe mikakati iliyoamuliwa na Baraza inafanyiwa kazi kwa ushirikiano wa Waheshimiwa Madiwani, mbunge na wataalamu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya MSALALA
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.