BARAZA LA MADIWANI LAPONGEZA JITIHADA ZA SERIKALI
Baraza la Madiwani na Wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala limepongeza jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Mhe. Dr John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutoa maelekezo mazuri ya matumizi
ya fedha za Ruzuku ya maendeleo (LGDG). Kauli hiyo ilitolewa na Baraza la Madiwani lililoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo
Mhe. Mibako Mabubu ambaye aliongeza kwa kusema "ni wazi kuwa miradi viporo iliyoibuliwa na jamii miaka iliyopita itapata suluhu katika
awamu hii kwa kuwa fedha zinazoletwa na Serikali kuu zimedhamiria kukamilisha miradi husika ili ianze kutoa huduma kwa wananchi".
Baraza hilo limefanyika leo tarehe 03.03.2018 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo. Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndugu
Simon Berege ameomba Baraza lipendekeze miradi ambayo ina uhitaji mkubwa kwa jamii sajali na kuangalia umbali wa huduma hiyo kwa lengo
la kuwezesha wananchi kupata huduma karibu na maeneo yao. Amesema Serikali ya awamu ya tano imetenga jumla ya Tsh: 851,382,999.00 kwa
Halmashauri ya Msalala ambapo hadi kufikia mwezi wa sita mwaka huu fedha hii itaingia katika akaunti za Halmashauri na kwenda moja kwa moja
katika miradi iliyopendekezwa. Sambamba na hilo Serikali kuu imetenga Tsh: 1,121,288,000.00 kwa mwaka wa fedha ujao 2018/2019.
Kwa upande wao Wah. Madiwani walipokea taarifa hizo kwa furaha na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha na kuzisimamia fedha hizo kikamilifu
katika maeneo yao ya utendaji ili kuweza kutekeleza lengo la Serikali. Baraza hilo lilipendekeza kukamilishwa kwa kituo cha Afya cha ngaya,
kukarabati miundo mbinu ya bomba la maji katika kata ya Segese, kujenga kituo cha kuzalishia mifugo katika kata ya Mega, Ukamilishaji wa
vyumba 12 vya madarasa katika kata za Mwakata na Kashishi, ukamilishaji wa nyumba 8 za walimu katika kata za Isaka, Busangi, Chela na Bulyanhulu,
ujenzi wa madarasa 3, nyumba 1 ya walimu na maabara 3 katika shule mpya ya Sekondari Kashishi. Shughuli hizi zitafanywa kwa fedha za mwaka huu
2017/2018 na miradi hii kuanza kutumika.
Kwa mwaka 2018/2019 Baraza hilo lilipendekeza shughuli za ukamilishaji na kuipandisha hadhi zahanati ya Isaka kuwa kituo cha Afya,
ukamilishaji wa majengo ya wagonjwa wa nje (OPD) katika kata za Mwanase, Mwalugulu na Busangi, Ukamilishaji wa vyumba 15 vya madarasa katika kata za
Lunguya, Segese, Mega, na Kashishi, na ununuzi wa ng'ombe 20, mbuzi 50 na kuku 500 . Hii ni baadhi ya miradi itakayotekelezwa.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.