Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Msalala limempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na timu yake ya Wataalamu kwa kufanya maandalizi vizuri ya makisio ya bajeti kwa mwaka 2018/19. Maandalizi hayo yamewezesha wajumbe kusoma bajeti hiyo kwa urahisi na kutoa michango yao kwa ufasaha. Kikao hicho kimefanyika kwa muda wa siku mbili tarehe 19/01/2018 – 20/01/2018 katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Akimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri kufungua kikao cha baraza hilo kaimu Mkurugenzi (W) ndugu Masatu Mnyoro alisema Bajeti ya mwaka wa Fedha 2018/2019 imelenga kuongeza uwekezaji katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo ujenzi wa maegesho katika kata za Isaka na Bugarama ili kuondoa utegemezi wa Halmashauri kutegemea mapato toka mgodi wa Bulyanhulu (ACCACIA), ambapo awali mgodi huo ulichangia asilimia 75 ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri.
Nae kaimu Afisa mipango (W) ndugu Conchesta Kabete alisema kwa mwaka wa Fedha 2018/19 Halmashauri ya Msalala imepanga kukusanya na kutumia jumla ya Tsh: 36,505,636,440 kutoka katika vyanzo mbalimbali kama inavyoonekana:
Na.
|
Chanzo cha Fedha
|
Makisio 2018/2019
|
1.
|
Mapato ya Ndani
|
5,195,632,500
|
2.
|
Ruzuku ya Kawaida (OC)
|
854,860,000
|
3.
|
Ruzuku ya Mishahara
|
23,446,903,848
|
4.
|
Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo
|
7,008,547,592
|
|
JUMLA
|
36,505,636,440
|
Sambamba na uwasilishaji wa Bajeti hiyo, Kaimu Afisa Mipango (W) huyo alisema bajeti hiyo imeandaliwa kwa kufuata miongozo mbalimbali ikiwemo Dira ya maendeleo ya Taifa, Mpango mkakati wa Halmashauri, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na sera mbalimbali za kisekta. Pia alitoa mrejesho wa bajeti ya mwaka wa Fedha 2017/2018 ambapo Halmashauri ilipanga kukusanya Jumla ya Tsh: 31,110,652,593 hadi kufikia mwezi wa kumi na mbili 2017 Halmashauri hiyo ilikusanya Tsh: 10,387,052,140.18 sawa na 33.5% ya makusanyo yake. Alitaja baadhi ya Mafanikio yaliyopatikana hadi mwezi Disemba 2017 kuwa ni ujenzi wa mabweni katika shule za Bulige na Ntobo, kuendelea kwa ujenzi wa jengo la makao makuu ya Halmashauri, kukamilika kwa mradi wa maji Igombe na Mhama kutoka bomba la Ziwa Viktoria, Kukamilika kwa miundombinu ya soko la kimkakati na ghala la kuhifadhia mazao ambalo lilifadhiliwa na MIVARF, kukamilika na kuanza kutumika kwa zahanati nne na kuendelea kwa taratibu za ujenzi wa Maji wa pamoja JWPP ambao umekusudia kupeleka maji katika kata ya Bugarama na Bulyanhulu, mradi huu takamilishwa ndani ya miezi 12 kuanzia Disemba 2017 na umefadhiliwa na Wizara ya maji, kampuni ya Accacia na Halmashauri ya Msalala.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Mibako mabubu alisema bajeti hiyo ni vema iangalie uwezekano wa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi ikiwemo ukamilishaji wa maboma yaliyokwama kwa muda mrefu ambapo kaimu Mkurugenzi (W) ndugu Masatu Mnyoro aliahidi suala hilo kulifanyia kazi kwa kuwa tayari Halmashauri imepeleka maandiko sehemu mbalimbali kutafuta wadau wa kukamilisha miradi hiyo, suala hili liliungwa mkono na wah. Madiwani wote na Mh. Ezekiel Magolyo Maige aliomba kupatiwa maandiko hayo sambamba na kupewa taarifa za mara kwa mara juu ya miradi yenye changamoto ili aweze kushiriki kutafuta wadau mbalimbali wa kimaendeleo.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.