Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga limempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo NDG. Khamis Katimba kwa uchapakazi wake kwani tangu uteuzi wake NDG.Katimba amekuwa akifanya kazi kwa vitendo na hivyo kuamsha mori kwa watumishi wengine kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa yeye binafsi anayaishi anayotaka yafanyike na ndo mana hufanya Vikao kazi vingi ngazi za Vijiji, Kata na Halmashauri hii yote ni kuhakikisha dhana ya Utawala bora inaenezwa kwa jamii nzima ya wakazi wa Halmashauri. Wakichangia hoja hii Wajumbe wa Baraza hilo wakiongozwa na Mibako Mabubu Mwenyekiti wa Halmashauri amesema NDG.Katimba ni mtu wa watu kwani yupo mbele muda wote iwe kwenye miradi ya maendeleo au zoezi la ukusanyaji mapato sambamba na utatuzi wa kero za wananchi.Nae Diwani wa Kata ya Bulyanhulu MHE.Shija Luyombya amemuelezea Mkurugenzi huyo kuwa ni msikivu kwani muda wote anapohitajika huenda kwa wakati Mungu amjalie Afya njema ili atutumikie wananchi wa Msalala.
Awali akiwakaribisha wajumbe wa kikao hicho na wageni waalikwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji(W)Bwana AbdulKadir Mfilinge amesoma Maelekezo ya Serikali yaliyotolewa katika kikao cha Wakurugenzi Watendaji na waziri wa OR TAMISEMI ambapo baadhi ya maagizo hayo ni kufanya maandalizi ya chaguzi za Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu kwa kuondoa dosari zote kabla ya uchaguzi, usimamizi wa Miradi,utatuzi wa kero,kutembelea miradi, ukusanyaji wa mapato sambamba na uondoaji wa migongano baina ya wenyeviti na Wakurugenzi.Kaimu Mkurugenzi huyo ameendelea kusema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali italeta fedha nyingi kutekeleza miradi ya sekta za Elimu na Afya na kuomba Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzisimamia kikamilifu. Baraza hilo limepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.
Nae Katibu Tawala Msaidizi(M) sehemu ya Menejimenti,ufuatiliaji na ukaguzi NDG.Ibrahim Makana amepongeza Halmashauri kwa kupata hati safi kwa mwaka 2023/2024 na kuitaka Halmashauri kufanyia kazi hoja zilizobakia ili zifungwe ofisi ya Katibu Tawala(M) inasubiri ili iunganishe majibu ya Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga na kuwasilisha siku ya Jumatatu 13-05-2024 sambamba na hili kila idara na kitengo kitumie vifungu vyake kwani bajeti ilipangwa kwa kila idara na kitengo.Kumbukeni kutenga fedha za mafunzo mara baada ya uchaguzi kwa viongozi,shughuli zinazoandikwa ziweze kupimika na hakikisheni makusanyo ya 60% ya miradi ya maendeleo na 10% ya wanawake,vijana,walemavu na watoto zinapelekwa kama ilivyopangwa.Mwisho fedha zote zinazokusanywa kupitia mfumo wa TAUSI zipelekwe benki siku hiyo hiyo zilipokusanywa ili kuondoa hoja za ukaguzi zisizokuwa na ulazima.
Baraza hilo limehitimishwa leo kwa wajumbe kutaka Mapato kukusanywa kwa hali yeyote ikiwemo mawakala kubadilishwa mageti mara kwa mara kwa lengo la kuondoa mazoea sambamba na kufanya doria za kustukiza maeneo yote yenye vyanzo vya mapato ya Halmashauri ili kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita ya utekelezaji miradi ya maendeleo kwa wakati kwani unapokuwa na nguvu kiuchumi maana yake utatekeleza miradi mingi kwa muda mchache.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.