baraza la madiwani la Halmashauri ya Msalala limejipongeza kwa kuwezesha Halmashauri hiyo
kukusanya mapato vizuri kwani hadi mwisho wa robo ya tatu, Halmashauri hiyo imefikisha 92%
ya lengo la kukusanya Tshs. 5,068,800,000 kwa mwaka 2022-2023. Pongezi hizi zimetolewa katika
kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani kilichofanyika leo katika ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Katika Kikao hicho pia imetolewa taarifa ya mapokezi ya vifaa vya kisasa katika Hospitali ya
Wilaya iliyopo katika kata ya Ntobo sambamba na kuitaka jamii ya wanaMsalala kutembelea Hospitali
hiyo kwani MHE.Rais mama Samia Suluhu anatambua shida wanazopata wananchi hivyo ameamua kujenga
maabara ya kisasa na kuweka vifaa muhimu sambamba na kutoa mafunzo baadae kwa wataalamu wa Afya ili
waweze kuvitumia vifaa hivyo, jamii inakaribishwa kupata huduma za Afya.
Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji Mhe. Joseph Manyara amelifahamisha Baraza la Madiwani
katika robo hii, Halmashauri imekamilisha ujenzi wa Zahanati 28 zipo tayari kuanza kutoa huduma kwa
wananchi na kumuomba Daktari wa Wilaya kuomba wataalamu toka wizarani sambamba na kupeleka wataalamu
walau wawili ili kuweza kutoa huduma ya Msingi kwa jamii kwani wananchi hulazimika kusafiri umbali
mrefu kufuata huduma, suala ambalo daktari wa Wilaya amekubaliana na hoja hiyo na kuahidi kulipatia
ufumbuzi kwa wakati.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Halmashauri ya Msalala
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.