Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Msalala limepitisha Taarifa za Hesabu za kufungia mwaka 2022-2023
katika ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo katika kijiji cha ntobo Wilayani Kahama.Akifungua kikao hicho
mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Mibako Mabubu ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta fedha
ndani ya Halmashauri na kuomba ushirikiano uliopo kati ya wataalamu na Waheshimiwa madiwani udumishwe
kwani maendeleo yanayoonekena yanatokana na ushirikiano uliopo.
Akiwasilisha hesabu za Halmashauri kwa mwaka 2022-2023, Zayana Mutabazi kwa niaba ya Mweka Hazina(W)
amesema ufungaji wa hesabu umetumia mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE)ambapo hadi kufikia mwishoni mwa
mwaka 2022-2023 Halmashauri ilikuwa na rasilimali zenye thamani ya Tsh. 40,972,700,781 ambapo kuna ongezeko
ambalo limetokana na kuongeza utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ununuzi wa mitambo,ujenzi wa nyumba,
majengo na miundombinu mbalimbali zenye mwelekeo wa rasilimali za kudumu.
Pia Halmashauri ilikusanya Tsh.5,400,764,033.04 sawa na 101% ya kukusanya 5,368,800,000 kwa mwaka 2022-2023 kutoka
kwenye mapato ya ndani.Halmashauri ilikusanya Tsh.37,145,427,709.47 ukijumuisha fedha za mishahara,wahisani mbalimbali,
Serikali kuu na mapato ya ndani.Halmashauri imetumia Tsh.34,863,587,600.47 na kuachia salio la Tsh.2,281,840,109.00 ambazo
ni fedha za TSA zinazosubiri maelekezo ya kuziondoa.
Wakichangia hoja,Mhe. benedicto Manwali diwani wa kata ya Lunguya,amesifia utendaji unaoonyeshwa na Mkurugenzi Mtendaji(W)
na timu yake ya wataalamu kwa kuiwezesha halmashauri kuvuka lengo la kukusanya mapato sambamba na kuwezesha kuondoa hoja
za ukaguzi ambazo hupelekea Halmashauri kupata hati chafu, hoja hii imeungwa mkono na baraza lote la Madiwani na kuomba
jitihada hizi ziwe endelevu ili wananchi wawezeshwe kufikia malengo na matarajio wanayoyahitaji.
Nae Katibu mwenezi wa CCM(W) ndg.Joakim Shimbila amepongeza madiwani hao na kusema wanasimamia vizuri ilani ya uchaguzi katika
maeneo yao kwani miradi inatekelezwa na kukamilika kwa wakati,hii inatokana na usimamizi wenu wa karibu endeleeni kuhakikisha
miradi inatekelezwa kwa viwango vya juu sambamba na fedha iliyotolewa. Mwakilishi wa Katibu Tawala(M) ndg.Baraka Bulayo ameishukuru
Halmashauri kwa kutulia na kutekeleza vizuri maagizo na kusimamia vizuri miradi na kuomba hali hii iendelee kwani maendeleo huja
kwa kuchapa kazi na kuelewana.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji(W) ndg.Mary Nziku amepokea shukrani zilizotolewa na viongozi mbalimbali na ameahidi kuendeleza
uhusiano mzuri baina ya watumishi na waheshimiwa madiwani kwani ndio msingi mkuu wa mafanikio haya,halmashauri imepata hati safi tangu
kuanzishwa kwake kutokana na kushirikiana katika kuhakikisha miradi inasimamiwa vizuri sambamba na kuwa na nidhamu kwenye matumizi ya fedha
za serikali.Sisi kama wataalamu tutaendelea kuwashauri vizuri waheshimiwa madiwani nanyi mda wowote mtutume tupo tayari kuwatumikia wananchi
na kuhakikisha ilani ya chama tawala tunaitekeleza kwa vitendo,amesema kaimu mkurugenzi huyo.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.