Baraza la Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga limeridhia na kupitisha mapendekezo ya Mpango wa uwajibikaji
wa Makampuni kwa jamii (CSR) kwa mwaka 2024.Kikao hicho kimehudhuriwa na waheshimiwa madiwani wote,mheshimiwa Mbunge,Wakuu wa
idara na Vitengo wa Halmashauri,wataalamu toka ngazi ya kata na vijiji,wawakilishi wa wataalamu toka idara ya maendeleo ya jamii
kutoka Mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu na wananchi kwa ujumla.
Akiwakaribisha wajumbe katika kikao hicho,Mkurugenzi Mtendaji(W) NDG.Khamis Katimba ameeleza maagizo ya Serikali yaliyotolewa katika
kikao chao na Waziri wa ofisi ya Rais,TAMISEMI MHE.Mohamed Omar Mchengerwa kuwa Halmashauri nchini zinapaswa kuhakikisha zinatumia
mfumo mpya ujulikanao kwa jina la TAUSI katika kukusanya mapato kwani mfumo huu umeondoa changamoto za upotevu wa mapato kwa kuzimba
mianya yote ya udanganyifu wa mapato.
Pia Halmashauri zihakikishe miundombinu iliyowekwa na Serikali inakuwa na miundombinu yote inayotakiwa ili kuwezesha miradi kutoa
huduma kwa wananchi kwa wakati,ametaja miongoni mwa miundombinu hiyo kuwa ni uwepo wa madawati katika shule za msingi na sekondari
ambapo amesema katika halmashauri ya Msalala yanahitajika madawati 8,712 viti na meza 4,902 ambapo yeye yupo tayari kuhakikisha
upungufu huu unapatiwa suluhisho.Agizo jingine ni kushirikiana na kuhakikisha shughuli za Halmashauri zinatangazwa tokea ngazi za
vijiji.
Mkurugenzi huyo amewataka wajumbe hao kupendekeza miradi yenye tija kwa jamii zao kwani mpango huu ni maalum kwa ajili ya shughuli
za kuwezesha jamii kujiendeleza kiuchumi, ametaja maeneo ya kipaumbele yaliyotolewa na uongozi wa Barrick Gold Mine kuwa ni maeneo ya
afya ambapo amesema watu wakiwa na afya njema inawawezesha kuendelea na shughuli za uzalishaji uchumi,eneo lingine ni elimu ambapo
watoto wakipatiwa elimu bora huleta ukombozi baadae kwa familia na taifa kwa ujumla.
Akiwasilisha mpango na bajeti ya uwajibikaji wa makampuni kwa jamii (CSR) Afisa mipango na Uratibu(W) NDG.Elkana Zabron amesema kwa mwaka
2023 fedha za uwajibikaji wa Makampuni kwa jamii (CSR) Halmashauri ilipanga kutumia Tsh.1,977,800,000 katika sekta za Afya na Elimu ambapo
hadi sasa Halmashauri imetumia Tsh.1,350,399,442.24.Ameitaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kupitia fedha hizi kuwa ni ujenzi wa mabwawa ya kunyweshea
mifugo katika kata ya Bulyanhulu,ujenzi wa ofisi ya kata Bulyanhulu,kukamilisha jengo la utawala, vyumba 2 madarasa na matundu ya vyoo 8 katika
chuo cha VETA kata ya Bugarama na ujenzi wa uzio stendi ya Isaka.
Kwa mwaka 2024 Halmashauri inatarajia kutumia Tsh.2,000,000,000.00 kutoka katika chanzo cha uwajibikaji wa makampuni kwa jamii(CSR) kinacholipwa na
mgodi wa barrick,Halmashauri ikishirikiana na wataalamu kutoka Kampuni ya Mgodi wa dhahabu wa Barrick-Bulyanhulu wamewezesha uibuaji wa vipaumbele.
Vipaumbele hivi vimezingatia muongozo wa uwajibikaji wa Makampuni wa mgodi huo ambapo utajikita kwenye maeneo ya uchumi na uzalishaji,Mazingira,
Kilimo na huduma za jamii ikiwemo elimu na afya.Aidha mpango huu utajikita katika kulipa madeni ya miradi iliyotekelezwa miaka ya nyuma na kutekeleza
maagizo ya serikali ambapo Halmashauri imetenga Tsh. 400,000,000 kuwezesha madawati, viti na meza kupatikana na Tsh. 200,000,000 kwa ajili ya kuongeza
vifaa tiba na kuajiri wataalam 16 wa idara ya Afya kupunguza ukosefu wa wataalamu katika sekta hiyo.
Nae Mbunge wa jimbo la Msalala Mhe.Alhaj Idd Kassim Idd ameitaka Halmashauri kuhakikisha mpango uliowasilishwa unatekelezwa kwa vitendo na kwa wakati
kwani fedha inayotolewa na Mgodi wa Barrick-Bulyanhulu si hisani bali ni takwa la kisheria kwa Kampuni hiyo kuwajibika kwa jamii inayoizunguka na akaipongeza
Halmashauri chini ya uongozi wa mwenyekiti Mibako Mabubu kwa kuongoza jamii kuibua miradi yenye mashiko kwa wananchi,ametaja baadhi ya maeneo ambayo Halmashauri
imepanga kufanyia kazi kuwa ni kuajiri wataalam wa afya kwenye maeneo ambayo Serikali haijapeleka wataalamu kwani Halmashauri imefungua zahanati 5 na mwezi
Januari 2024 itaongeza zahanati 8 na kupandisha hadhi zahanati za Segese na Bulige kuwa vituo vya afya.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Mboni Mhita amempongeza Mbunge wa jimbo la Msalala kwa kuliwakirisha vema jimbo lake bungeni kwani kila kona ya
Halmashauri ya Msalala miradi ya maendeleo inatekelezwa kutokana na jitihada za Mbunge za kuiomba Serikali yetu tukufu inayoongozwa na Rais kipenzi cha watu
mama yetu Dr.Samia Hasain Suluhu na kuahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa Halmashauri hiyo kuwezesha ilani ya CCM kutekelezwa kwa ufasaha,ameongeza
kusema hana tatizo na Halmashauri hiyo kwani siku zote Halmashauri ya Msalala hutekeleza miradi ya wananchi kwa ubora na viwango vya juu hii yote inatokana
na uongozi thabiti wa Mwenyekiti wa Halmashauri na baraza lake bila kumsahau Mkurugenzi shupavu NDG.Khamis Katimba hakika unaupiga mwingi katika kuhakikisha
maagizo ya Serikali ya awamu ya sita yanatekelezwa kwa wakati.
Nao baadhi ya madiwani akiwemo Mhe.Shija diwani wa Kata ya Bulyanhulu ameitaka Halmashauri kutembelea maeneo yaliyopendekezwa kabla ya utekelezaji na kutengeneza BOQ inayoendana na uhalisia
wa bei za soko,suala ambalo limeungwa mkono na Mhe.Benedict Manwali diwani wa kata ya Lunguya na Mhe.Masanja diwani wa kata ya Mwanase ameipongeza mpango huo kwa kuwa wananchi wa kata yake
wanahangaika kufuata huduma katani hivyo uwepo wa zahanati nyingine utawezesha wananchi kupata huduma karibu.
Kikao hiki kimehitimishwa na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Mibako mabubu kumhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe.Mboni Mhita kuwa maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa na
Serikali ya awamu ya sita yanatimizwa kwa wakati kwani Mkurugenzi Mtendaji(W) na timu yake ya wataalam ni wasikivu na wachapakazi hivyo yale yote yaliyopitishwa kwenye mpango
wa CSR kwa mwaka 2024 yatatekelezwa na kuwaomba wananchi wa Halmashauri ya Msalala kuilinda na kuitunza miradi iliyokwisha tekelezwa kwani fedha ya Serikali ni fedha yao hivyo
tuithamini miradi yetu.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.