Kauli hii imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira Mhe. Gerard Mwanzia wakati wa kikao cha kujadili na kupitia bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20 katika ukumbi wa Halmashauri ya Msalala. Mhe, Mwanzia amesema kutokana na hali halisia ya mapato ndani ya Halmashauri ni vema vyanzo vya mapato vilivyopo vikaboreshwa Zaidi ili kuweza kuwa na uhakika wa kukusanya ushuru ambapo amesema katika bajeti hii Halmashauri ni lazima iweke bajeti ya kujenga uzio katika mnada wa Bulige, Masabi na baadae Bugarama.
Suala ambalo limetolewa ufafanuzi na mkuu wa idara ya Mifugo na Uvuvi DR. Ntanwa Kilagwile ambapo amesema bajeti imezingatia ushauri kwani katika mpango wa bajeti kwa mwaka 2019/20 Halmashauri imepanga kujenga uzio katika mnada wa Bulige na kuboresha miundombinu ya gulio la kakola sambamba na kufanya ukarabati wa majosho mawili. Halmashauri inalazimika kukamilisha ujenzi huo kidogo kidogo kutegemeana na upatikanaji wa Fedha.
Kwa upande wake Kaimu Afisa Mipango (W) ndugu Elkana Zabron akitoa taarifa ya bajeti kwa wajumbe wa kamati hii amesema katika mpango na bajeti ya 2019/20 Halmashauri imepanga bajeti kulingana na hali halisi ya makusanyo yake kwani katika mwaka 2017/18 Halmashauri ilipanga bajeti kulingana na maoteo suala ambalo lilisababisha Halmashauri kuwa miongoni mwa Halmashauri zilizofanya vibaya katika ukusanyaji mapato hii ilitokana na kukadiria mapato yasiyokusanyika kutoka mgodi wa Bulyanhulu ambao ulipunguza uzalishaji na hivyo kuathiri mapato ya Halmashauri ambayo yalichangia Zaidi ya 75% ukijumlisha na ushuru unaolipwa na makampuni yanayofanya kazi na mgodi.
Wajumbe hao waliitaka Halmashauri ianze kupimia watu viwanja kwa kutumia makampuni kwani viwanja ni chanzo kingine kizuri cha mapato sambamba na kuwaomba TARURA kuchukua mahitaji ya matengenezo ya barabara kutoka Halmashauri kwani itasaidia kutatua maeneo korofi ya barabara kwa kuwa Halmashauri inatambua maeneo hayo.
Nae Mkurugenzi Mtendaji Bwana Simon Berege amesema tayari Idara ya Ardhi na Maliasili imeshaanza kupima viwanja katika kata za Ntobo, Mega na segese na Halmashauri inategemea kupata fedha toka wizara ya Ardhi na Maliasili kwa ajili ya upimaji wa viwanja ndani ya Halmashauri na hivyo itashirikisha makampuni ili maeneo mengi yaweze kupimwa, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema pia Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa Halmashauri makini Tanzania kwani iliandaa maandiko mbalimbali ambayo Serikali iliziomba Halmashauri nchini ziandae kulingana na mahitaji yao ili Serikali kuu iweze kuleta fedha ya kukamilisha miradi hiyo hivyo tunategemea kupokea fedha za kukamilisha miradi mbalimbali ndani ya kata zetu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
MSALALA
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.