Elimu ya maadili ya viongozi wa Umma imetolewa leo tarehe 30/10/2018 na mratibu wa Sekritarieti ya maadili ya viongozi wa umma wa kanda ya Magharibi ndugu hamad Bakari Sharia ambapo amesema kwa kiongozi wa umma kuwa na mali sio dhambi ila ni lazima ueleze ni namna gani umezipata mali hizo na ndiyo maana Serikali imeona ni vema kutoa fomu za kujaza kila mwisho wa mwaka mali wanazomiliki viongozi wa umma. Ni takwa la kisheria kujaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa wakati katika taasisi yako na baadae kutumwa makao makuu ya Sekritarieti ya Maadili ya Umma ambapo taarifa hizi huingizwa kwenye kazidata na hutunzwa kwa usiri mkubwa. Elimu hii imetolewa kwa Waheshimiwa Madiwani na Wakuu wa idara wa Halmashauri hiyo.
Kwa upande wao Viongozi wa Halmashauri wameshukuru kwa kupewa elimu hiyo na kwa kuelekezwa vizuri na hivyo kuahidi kujaza fomu za tamko la maadili la mali na madeni kwa wakati kwani awali walijaza pasipo kupewa maelekezo hivyo viongozi hao watafanya kazi kulingana na sheria, kanuni na taratibu zilizopo na kujiepusha kuwa na mgongano wa kimaslahi kama mwezeshaji wa elimu hii alivyoelekeza. Lengo la maelekezo haya ni kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa pasipo kubaguliwa na kwa wakati kwani Serikali ya awamu ya tano ni Serikali inayotetea maslahi ya wananchi hivyo wafanyakazi wa Serikali wakitimiza wajibu wao lengo hili litatimia.
Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Msalala
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.