Halmashauri ya Wilaya ya Msalala imeanza maandalizi ya kuandaa mpango mkakati wa namna bora ya kukabiliana na majanga pindi yanapotokea kwani majanga siku zote hutokea bila taarifa hivyo Halmashauri ikishirikiana na wadau wake OXFARM ambaye anajishughulisha na kuongeza thamani ya mazao sambamba na kuwatafutia masoko wakulima kwa lengo la kukuza kipato cha wananchi wanaoishi kanda ya ziwa na CABUIPA ambalo linajihusisha na kujengea uwezo kamati za maafa za Halmashauri na baadae kamati hii ikishirikiana na shirika la CABUIPA kuieneza elimu hiyo kwa jamii.
Akiitambulisha shirika la CABUIPA kwa kamati ya maafa ya Halmashauri mratibu wa mradi wa KAMA amesema CABUIPA imejipanga kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinakuwa na mpango mkakati mbadala wa kukabiliana na majanga, na kwa sasa shirika linafanya majaribio ya mradi huo katika mkoa wa Shinyanga katika Halmashauri za Msalala na Kishapu lengo ni kuzifikia Halmashauri zote nchini. Ndugu David Rwegoshora ametaja baadhi ya malengo ya mradi huo kuwa ni kujengea uwezo jamii ili ziweze kujikinga pindi maafa yanapotokea, Jamii ifahamu vyanzo, athari na njia za kujikinga nazo na mwisho jamii ikishirikiana na wadau waweze kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.
Nae Kaimu mkurugenzi Mtendaji DR. Ntanwa Kilagwile amewashukuru wadau wa OXFARM na CABUIPA kwa kuchagua eneo la Halmashauri ya Msalala kuanza kufanya kazi nao kwani upatikanaji wa mpango mkakati huo utasaidia Halmashauri kuwa tayari muda wote kwa kuwa tayari mipango itakuwepo sambamba na jamii kuelewa namna ya kufanya pindi maafa yanapotokea na kuahidi kutoa ushirikiano ili mpango mkakati huo wa maafa ukamilike mapema.
Kwa upande wao washiriki wa semina hiyo walitoa shukurani zao kwa wadau kwa kuona umuhimu wa kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuondoa vifo visivyo vya lazima kwa kutoa elimu juu ya kujikinga na majanga kwani kuelewa vyanzo, athari na njia za kujikinga kutaiwezesha jamii kujikinga na majanga pindi yanapotokea na kuitaka jamii kuhudhuria kwa wingi pindi semina hizi zitakapoanza kutolewa kwani Halmashauri imejipanga vizuri kuweza kushirikiana na wadau wake kuhakikisha elimu hii muhimu inawafikia wananchi wengi waishio vijijini.
Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Msalala.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.