Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama leo 08.01.2024 imepitisha Mpango mkakati wa miaka 5 (2021/2022 hadi 2025/2026) kwa kukutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo
waliopo ndani na nje ya Halmashauri hiyo. Awali akiwakaribisha wajumbe katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji NDG.Khamis Katimba amesema mchakato wa kuandaa mpango
huo uliandaliwa miaka 3 iliyopita na kuanza kutumika hivyo wadau wana nafasi nzuri ya kuchangia kwa kuwa tayari mpango huo wanauishi.Amewataka wajumbe hao kuwa huru
katika kukosoa,kutoa mapendekezo katika hoja zao lengo likiwa ni kutoa huduma nzuri na yenye tija kwa wananchi.
Katika Mpango Mkakati huo kuna malengo na njia za kuwezesha kufikia malengo hayo ambapo jumla ya idara na vitengo 19 vimewasilisha malengo yao na kuonesha mafanikio
yaliyokwisha fikiwa tangu kuanza kufanya kazi kwa mpango mkakati huo,baadhi ya malengo hayo ni kuwezesha wananchi wa Halmashauri ya Msalala kufanya kilimo cha kibiashara
kwani wakazi wa eneo hili ni wakulima na wachimbaji sambamba na kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa wajasiriamali na wawekezaji kufanya biashara ndani ya Halmashauri.
Pia Halmashauri kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya Halmashauri.
Nae Mhe.Alhaj Idd Kassimu Idd Mbunge wa Jimbo la Msalala amemshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu kwa kuleta fedha nyingi ndani ya
Halmashauri kwani Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa Halmashauri zilizopokea fedha zote za kutekeleza miradi ya maendeleo na ni Halmashauri ya kwanza kupata fedha nyingi
mkoani Shinyanga.Ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa kupitia fedha hizo kuwa ni ujenzi wa vituo vya afya katika kata za Isaka,Mwalugulu,Segese,Bulige,Mwanase ambapo zaidi
ya Tsh. bilioni 2.5 zimetumika kukamilisha vituo hivyo.Halmashauri pia imekamilisha zahanati 24 na zimeanza kutoa huduma hii yote ni jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu
ya 5.
Mbunge huyo amewaomba wananchi kuwa na subra kwenye ujenzi wa barabara ya Kahama Kakola kwa kiwango cha lami kwani ofisi yake ikishirikiana na ofisi ya mkuu wa Wilaya na mkoa
kwa ujumla wameiomba Serikali kuondoa tozo kwenye mradi huo ambapo jumla ya tozo ni bilioni 17 ambapo tozo hii ikiondolewa itawezesha kuunganishwa Halmashauri ya Nyagwale na
kakola kwa kiwango cha lami hivyo viongozi wenu tunapambana kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wetu.Mwisho Mbunge huyo ametoa rai kwa jamii kuwapeleka watoto wao shuleni
kwani halmashauri imekamilisha miundombinu yote inayohitajika katika ujifunzaji.
Kwa upande wake OCD wa Wilaya ya Kipolisi ya Msalala, Afande Masome ameitaka menejimenti ya Halmashauri ya Msalala kuweka kipaumbele kwenye suala la ulinzi kwani maendeleo hayawezi
kufikiwa pasipo kuwa na amani hivyo katika mpango mkakati huu wekeni kipaumbele cha kwanza ulinzi kwani Halmashauri ni kubwa lakini vituo vya polisi ni 4 kati ya kata 18,ni vizuri
tuanzishe vituo vya polisi hasa katika kata za Bulige na kumalizia kituo cha polisi Isaka kwani Halmashauri ya Msalala ina vyanzo vingi vya mapato hivyo tukiimarisha ulinzi na usalama
ndani ya Halmashauri mapato pia yataongezeka.
Akiwasilisha mada ya mpango na Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2024/25 Afisa Mipango wa Halmashauri ya Msalala Bwana Elkana Zabron amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 Halmashauri imepanga
kukusanya Bilioni 5.5 ambapo kuna ongezeko la milioni 500 kutoka bajeti ya mwaka 2023/2024,ongezeko hili litatokana na kufunguliwa kwa stendi ya mabasi ya Isaka,kuboreshwa kwa mazingira
ya kukusanyia ushuru wa mazao,tozo za minada na maboresho ya ukusanyaji mapato toka kampuni zinazofanya kazi na mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu ambapo Halmashauri inategemea kukusanya mapato
hayo kila mwezi.
Wadau Mbalimbali wamechangia hoja katika kikao hiki, ambapo bwana Kizito Mtendaji wa kata ya Isaka ameiomba Halmashauri kukaribisha wawekezaji kujenga maghala ya kuhifadhia mpunga na
mashine za kukoboreshea mpunga kwani Halmashauri ya Msalala inazalisha mpunga kwa wingi na kuzinufaisha Halmashauri jirani za Shinyanga vijijini na Manispaa ya Kahama ambapo mpunga hupelekwa na
kuziwezesha Halmashauri hizo kujipatia ushuru,suala ambalo limeungwa mkono na Bertha meneja wa kampuni ya Dofra, kampuni inayojihusisha na utoaji wa vifaa vya kilimo kwa wakulima na kununua
mazao ambapo ameitaka Halmashauri kuongeza mageti hasa maeneo yenye njia pacha sambamba na kuwezesha wagani kutembelea mashamba darasa yaliyoanzishwa.
Mdau mwingine ni Mhe.Dismas Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Lunguya ambaye ameiomba Halmashauri kupima maeneo yote yanayomilikiwa na Serikali na hasa maeneo ya Mahakama kwani kuna mradi wa
wa kimataifa wa kujenga mahakama,kigezo kikubwa ni ardhi iwe imepimwa hivyo Halmashauri iwezeshe suala hili sambamba na kuwezesha vitendea kazi kwa ofisi za watendaji wa kata/vijiji na
kuyajengea uwezo mabaraza ya ardhi ya kata kwani mabaraza haya yamekuwa yanaingilia shughuli zisizowahusu.
Akijibu hoja mbalimbali zilizoulizwa na wadau Mkurugenzi Mtendaji(W) amesema katika Bajeti tunayoitekeleza Halmashauri imepanga zaidi ya milioni 18 kukamilisha jengo lililopo kituo cha polisi
Ilogi na katika bajeti ya mwaka 2024/2025 pia imetenga fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo vya polisi ndani ya Halmashauri huku kipaumbele kikiwekwa katika kata ya Isaka kwani ni eneo
la kimkakati ambalo linategemewa kuingiza fedha nyingi ndani ya Halmashauri hivyo suala la uwepo wa usalama litavutia wawekezaji wengi kuwekeza ndani ya Halmashauri, hii inaendana na kuwezesha
ofisi za wenyeviti na watendaji wa kata na vijiji kupewa fedha za kuendeshea ofisi zao na kuwezesha maeneo yote ya Serikali kupimwa kwa awamu.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala Mhe.Mibako Mabubu amewashukuru wadau wa maendeleo ya Halmashauri kwa kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao juu ya maendeleo ya shughuli za
Halmashauri na kusema michango waliyoitoa atahakikisha Mkurugenzi Mtendaji anafanyia kazi yeye na watumishi wote wa Halmashauri sambamba na mwenyekiti huyo kufanyia kazi yaliyoagizwa yeye na waheshimiwa
madiwani wenzake kwa kuwa watumishi na madiwani wamechaguliwa na wananchi hivyo ni lazima tufanye kazi kwa niaba yao.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.