Halmashauri ya Msalala imefanya kikao chake cha kumaliza mwaka 2016/17 ambapo wah. Madiwani wote 24 na mbunge mh. Ezekiel M. Maige walihudhuria kikao hicho, pia wakuu wa idara na vitengo , kamati ya ulinzi na usalama ( W) , viongozi toka mkoani, viongozi wa dini na siasa, wanachi na wana habari mbalimbali walihudhuria kikao hicho.
Akiongea katika kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji ( W ) ndg. Simon Berege alisema Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa Halmashauri vinara nchini kwa ukusanyaji mapato ambapo Halmashauri kupitia idara ya Fedha na Biashara imeiwezesha Halmashauri kuvuka lengo kwa kukusanya mapato ya ndani kwa thamani ya Tsh. 1,978,236,770 sawa na 111% kutoka lengo la kukusanya 1,259,548,759.
Akichangia mada Mh. Matrida Msoma diwani wa kata ya Ikinda aliipongeza Halmashauri na kuitaka kuboresha huduma za vyoo hasa katika maeneo ya minada na magulio pia idara ya Ardhi na Maliasili ipime na kutoa hati kwa maeneo yote ya vitega uchumi vya Halmashauri.
Akichangia hoja hii Mweka hazina wa Halmashauri bw. Masatu Mnyoro alisema tayari Halmashauri imeshachukua hatua kwa kuanza kujenga vyoo katika kata za Isaka na Bulige na kuahidi kutekeleza suala hilo katika kata za Ikinda na Bulyanhulu katika awamu ya pili ya Ujenzi. Nae mkuu wa idara ya Ardhi na Maliasili ndg. Zabrone donge alisema Halmashauri imeshaanza kupima maeneo yote ya Halmashauri na imeanzia katika kata ya Bulige na baadae itaenea katika kata zote.
Sambamba na hoja hii wajumbe wa baraza la madiwani Halmashauri ya Msalala walitaka kufahamu hatima ya barabara zao ambapo Mkurugenzi Mtendaji ndg. Simon Berege alisema kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 barabara zote zimekabidhiwa kwa mamlaka ya wakala wa barabara vijijini na mijini ( TARURA) ambapo watumishi wawili toka Halmashauri ya Msalala wameazimwa na TARURA ili kuweza kuwezesha Taasisi hii kufanya kazi zake. Na hivyo kuomba wajumbe kuwa wavumilivu kwa kuwa muda si mrefu Taasisi hiyo itaanza kutekeleza majukumu yake.
Akichangia hoja hii Mh. Frola Sagasaga aliiomba Serikali pindi TARURA itakapoanza kazi zake iikumbuke barabara ya Mwankima _ Mwalugulu kwa kuwa haikutengenezwa kwa kiwango kinachotakiwa, nae Diwani wa kata ya Ikinda aliiomba TARURA kuangalia uwezekano wa kuitengeneza barabara ya Ikinda kwa kuwa inaunganisha Halmashauri ya Msalala na Mbongwe.
Suala la Huduma ya Afya na Elimu nalo lilijadiliwa katika kikao hiki ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alisema Halmashauri ya Msalala imekuwa kinara katika utoaji wa huduma za afya nchini na hivyo kuviwezesha vituo vyake vya kutolea huduma kuweza kujiendesha vyenyewe kimapato kupitia miradi ya RBF ambapo ukarabati wa majengo na miundo mbinu za vituo hivyo hufanyika sambamba na ununuzi wa madawa na kulipa gharama za walinzi. Akichangia mada hii daktari mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala bw. Hamad Nyembeah alisema katika mwaka wa Fedha 2016/17 Halmashauri iliweza kufungua Zahanati 6 na kituo cha Afya 1 na katika mwaka huu wa Fedha Idara ya Afya Jinsia wanawake na watoto imejipanga kuendelea kufungua kwa maeneo yaliyosaliosalia. Hija hii ilichangiwa na Diwani wa viti maalumu Mh. Angela Paul ambaye alitaka kufahamu ni lini Wah. Madiwani watapatiwa Vitambulisho vya Bima ya Afya na wazee kutambuliwa, Akijibu swali hilo Mkurugenzi Mtendaji Bw. Simon Berege alisema mara baada ya kikao hicho Wah. Madiwani wote wachukue fomu za NHIF wazijaze na kesho yake kuzikusanya tayari kwa kuzipeleka Mkoani kwa lengo la kupatiwa kadi zao mapema kwa kuwa Afya ndio msingi wa maendeleo ya mtu.
Nae Diwani wa Segese Mh. Joseph Manyara aliishukuru Serikalio ya awamu ya tano kwa kuwezesha shule za Sewkandari za Halmashauri ya Msalala kuwa na vifaa vya kutosha vya maabara na hivyo kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa Vitendo.
Sambamba na hoja hii mkurugenzi Mtendaji ( W) Bw. Simon Berege alitoa mrejesho wa Bajeti kwa mwaka 2017/18 kuwa Halmashauri imejipanga kuandika maandiko kwa ajili ya kutafuta wahisani watakaosaidia kukamilisha huduma mbalimbali ndani ya Halmashauri pia kubuni vyanzo vipya za kukusanya ushuru kwa kuwa ushuru uliokuwa unapatikana kutoka Mgodi wa Acacia kutokana na Maknikia kwa sasa umesitishwa. Mkurugenzi huyo aliongeza kwa kusema katika kipindi cha mwaka 2016/17 halmashauri ilikusanya fedha zaidi ya Bilioni 1.33 ya makusanyo ya 2015/16 ambapo ni sawa na 35% ya makusanyo ya mwaka huo. Kati ya makusanyo yote 66% ya makusanyo hayo yalitumika katika shughuli za miradi ya maendeleo ikiwemo ukamilishaji wa maboma ya Zahanati na shule katika kata mbalimbali ndani ya Halmashauri hiyo.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.