Kikao cha kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango cha Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kimepongeza jitihada zinazofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kuwahudumia wananchi, akimkaribisha mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mibako mabubu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo bwana Simon Berege alitoa taarifa ya kuwa “ Halmashauri ya Msalala ni miongoni mwa Halmashauri 50 nchini zilizopata mgao wa gari za kubebea wagonjwa wa dharula (Ambulance). Gari hilo limepangwa kwenda katika kituo cha Afya cha Bugarama kwani wakati wa ziara ya waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Walemavu na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu aliahidi kukiletea kituo hicho gari la dharula la kubeba wagonjwa. Sambamba na hilo Mkurugenzi Mtendaji huyo aliwafahamisha wajumbe wa kikao hicho kuwa Halmashauri ya Msalala imejipanga kutengeneza eneo la maegesho la magari makubwa Isaka ambapo Serikali kuu nayo imechangia fedha kwa ajili ya shughuli hiyo hivyo kuwaomba wananchi wa maeneo jirani na Isaka kuchangamkia fursa ya ajira pindi ujenzi huo utakapoanza. Mkurugenzi Mtendaji (W) ndugu Simon Berege amesema katika mwaka wa Fedha 2017/18 miradi mingi itatekelezwa kupitia fedha za mapato ya ndani na Fedha za Serikali kuu. Ametaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni Ujenzi wa Maegesho ya Malori Isaka, Ujenzi wa Machinjio ya kisasa Isaka, Usambazaji wa Miundo mbinu ya maji katika vijiji vya Kakola, Bugarama, Ilogi na Mradi wa maji wa ziwa Victoria kutoka Nduku _Busangi, Nyamigege, Kisuke, Gula, Ntundu, Chela, Ntobo, Masabi na eneo la Makao makuu. Wajumbe walipokea taarifa hizo na kupongeza jitihada zinazofanywa na Mkurugenzi Mtendaji akishirikiana na Serikali ya awamu ya tano kwa kujali maendeleo ya wananchi kwani upatikanaji wa huduma hizi utaondoa changamoto ya ukosefu wa maji katika maeneo mengi ya Halmashauri ya Msalala.
Suala jingine lililoongelewa katika kikao hicho ni kupunguzwa kwa bajeti ya mwaka 2018/19 kutoka Tsh. 4,419,679,950 na kuwa Tsh. 2,800,959,950 kutokana na kupungua kwa ushuru wa huduma kutoka mgodi wa Bulyanhulu pamoja na makampuni yanayofanya kazi na mgodi huo kwani Meneja wa Mgodi wa Bulyanhulu ndugu Benedict Busunzu amethibitisha hayo kupitia barua yake yenye kumbu namba BGML/600/1843/CORP ya tarehe 22 /01/ 2018 kuwa “ Mgodi umepunguza uzalishaji kwa 80%. Maelezo hayo yametolewa na Mweka Hazina (W) ndugu Edward Mnyoro wakati wa kikao hicho. Ndugu Edward Mnyoro ameendelea kutaja sababu zingine za kupunguza bajeti hiyo kuwa ni tamko la Mhe. Rais la kutokutoza ushuru kwa wafanyabiashara wadogo, Ukusanyaji wa ushuru wa mabango kuhamia mamlaka ya Mapato (TRA), Ada ya zabuni kuhamia mamlaka ya barabara Vijijini (TARURA) na 30% ya kodi ya Ardhi kutorudishwa Halmashauri.
Wajumbe walishauri miradi hiyo ianze mara moja pindi pesa zitakapopatikana ili kuweza kutatua mapema shida za Wananchi walio wengi kwani asilimia kubwa ya wananchi huishi vijijini. Nae Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mibako Mabubu akifunga kikao hicho aliomba wananchi kutoa ushirikiano kwa mwekezaji yeyote atakayetaka kuwekeza ndani ya Halmashauri kwa kuwa kufanya hivyo kutaongeza pato la Wana Msalala
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.