Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Tellack amependekeza miradi itakayozinduliwa na kuonwa na Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018/19, Mkuu wa mkoa huyo ametoa mapendekezo yake wakati wa ziara ya kukagua miradi iliyopendekezwa na Halmashauri. Mkuu wa Mkoa amefuatana na Katibu tawala (M) ndugu Albert Msovela, Mkuu wa Wilaya Ya Kahama ndugu Anamringi Macha, Katibu Tawala (W) ndugu Timothy Ndanya, vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wa idara na vitengo wa Halmashauri hiyo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa amependekeza miradi ya maji kakola Bugarama, ujenzi wa wodi za wagonjwa katika kituo cha afya Bugarama, uwezeshaji vijana, utunzaji mazingira, uzinduzi wa vyumba sita vya madarasa ya shule ya msingi segese, kuona daraja linalounganisha kata za Ngaya na Kinaga, na shughuli za wajasiriamali.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa huyo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama ndugu Anamringi Macha amesema wilaya inajitahidi kuhakikisha miradi yote yenye mapungufu inakamilika na kuanza kutoa huduma kwani ndilo lengo la Serikali ya awamu ya tano kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa ufanisi na wakati na kuahidi kufuatilia kwa ukaribu akishirikiana na timu ya wataalamu wa Halmashauri ya Msalala.
Mwenge wa Uhuru utapokelewa kimkoa katika Halmashauri ya Msalala iliyopo wilayani Kahama tarehe 08/05/2019 na kukimbizwa katika kata za Bulyanhulu, Bugarama, Segese na Ngaya na mkesha kufanyika katika kata ya Bulige. Tarehe 09/05/2019 Mwenge wa uhuru utakabidhiwa Halmashauri ya Ushetu na baadae utakimbizwa katika Halmashauri ya Mji wa Kahama siku ya tarehe 10/05/2019
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano.
Halmashauri ya Msalala.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.