Mkuu wa Wilaya ya Kahama ndugu Anamringi Macha leo amewataka wazazi kuwekeza kwenye Elimu kwa kuwawezesha watoto wao kwenda shule kwa kuwanunulia madaftari, nguo za shule na viatu sambamba na kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwani matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi uliofanyika mwaka jana Halmashauri ya Msalala watoto wamefaulu kwa 76.63% na hivyo kuleta changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa 73 ndani ya Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama amesema hayo katika kikao kazi kilichowakutanisha Mkurugenzi Mtendaji (W), Kaimu Afisa Elimu bwana Seleka Ntobi, Afisa Taaluma Sekondari, Katibu Tarafa , watendaji wa kata za Bulige, Chela, Busangi , Mwanase na Kashishi, Waheshimiwa Madiwani wa kata hizo, watemi wa sungusungu, wenyeviti wa vijiji na watendaji wa vijiji. Kikao hiki kimefanyika katika kata ya Bulige ambapo lengo la kikao kazi hiki ni kujadili namna ya kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa uliopo ambapo mkuu wa Wilaya amesema Halmashauri ifanye jitihada zake zote kuhakikisha watoto wote waliofaulu mtihani wanapata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza na kuwaomba Wah. Madiwani kufikisha ujumbe kwa wananchi ili wachangie nguvu zao kwa kujenga maboma na Serikali imalizie lengo ni kuwawezesha watoto wetu waliofaulu mtihani kuendelea na masomo. Ninawaomba wananchi “ Jengeni maboma na sisi Serikali tumalizie ili watoto wetu wasome”.
Akisoma taarifa ya ufaulu mbele ya mwenyekiti wa kikao kazi hicho Kaimu Afisa Elimu Sekondari (W) amesema jumla ya wanafunzi 4935 walifanya mtihani waliofaulu na kuchagiliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni wanafunzi 3717 sawa na 76.63% kati yao 19 wamechaguliwa kwenda nje Halmashauri ya Msalala. Hivyo kuna upungufu wa vyumba vya madarasa 73 kwa Halmashauri nzima, pia pana upungufu wa meza na viti, matundu ya vyoo hivyo naomba kila kiongozi aone namna ya kufanya ili tuweze kutekeleza agizo la mkuu wetu wa Wilaya kwani elimu ndiyo ufunguo wa maisha.
Nae Mkurugenzi Mtendaji (W) ndugu Simon Berege amesema ukamilishaji wa maboma utaangalia sehemu ambapo wananchi watakapokuwa wameonyesha jitihada zao kwakukamilisha boma/maboma mapema na kuahidi Halmashauri kukamilisha maboma hayo haraka ili yaanze kutumika na ametoa muda wa miezi miwili hadi kufikia mwezi wa tatu wanafunzi wawe tayari ndani ya madarasa hayo. Amewataka viongozi hao kuwa mabalozi wazuri kwa wananchi ili wawezekuchangia ujenzi huo wa maboma sambamba na kuomba mashirika ya dini na yasiyoya kidini, wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia jitihada hizi kwani elimu ni urithi pekee kwa familia nyingi hasa zenye kipato kidogo.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
MSALALA
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.