Leo mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha amewaongoza wadau wa maendeleo katika kata ya Bugarama kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na samani zake pamoja na matundu ya choo, harambee hiyo imefanyika katika ukumbi wa mtendaji wa kata hiyo. Awali Mtendaji wa kata hiyo Bi. Prisca Pius akisoma risala kwa mgeni rasmi amesema shule ya sekondari Bugarama ina upungufu wa vyumba vya madarasa 9, matundu ya choo 35, meza 218 na viti 316 na tayari jitihada mbalimbali za kupunguzaau kuondoa upungufu huu zimeanza kufanyika kupitia Ofisi ya kata.
Katika msafara huo Mkuu wa Wilaya huyo ameongozana na Mkurugenzi Mtendaji (W) ndugu Simon Berege, Kaimu Afisa Elimu Sekondari ndugu Seleka Ntobi, Afisa Maendeleo (W) bi. Aliadina peter, Kaimu Afisa Biashara bwana Machota longido kutoka ngazi ya Halmashauri. Pia walikuwepo Wah. Madiwani wa kata hiyo, Mhe. Izengo na Mhe. Prisca Msoma diwani viti maalum kata ya Bugarama, Bi maendeleo ya jamii ngazi ya kata, Mtendaji wa kata na vijiji . Katika harambee hiyo jumla ya Tsh. Milioni nne zilipatikana ambapo mkurugenzi Mtendaji aliwaomba wajumbe wa kikao kazi hicho watoe vifaa vyenye thamani sawa na ahadi zao badala ya kuchangia fedha.
Katika Harambee hiyo makampuni mbalimbali yanayofanya kazi na mgodi wa acacia yametuma wawakilishi kusikiliza ujumbe wa kikao kazi hicho na baadae kuona namna nzuri ya kuchangia kwa lengo la kuwezesha jamii ya Bugarama kuwa na maendeleo kupitia kuwasomesha watoto katika mazingira bora kwani elimu ndiyo urithi pekee ambao unaweza kumwezesha mtu kupambana na changamoto za maisha zilizopo kwa kumsaidia kupata suluhisho la changamoto hizo. Wananchi wasitegemee elimu kwa ajili ya kupata ajira bali wategemee elimu kwa ukumbozi na hazina ya baadaye kwani elimu ndio ufunguo wa maisha.
Katika ziara hii Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha amepata fursa pia ya kuongea na vijana wajasiriamali ambapo amewasisitiza kuwekeza kwenye elimu kwa kuwawezesha watoto wao kwenda shule kwa kuhakikisha wanawapatia mahitaji muhimu kama nguo, viatu, kalamu , madaftari na chakula sambamba na kuiomba jamii kusaidia kuongeza miundombinu mashuleni kwani kutegemea Serikali pekee ni kujicheleweshea maendeleo kwani Serikali tayari inapeleka fedha mashuleni moja kwa moja hivyo jamii ina jukumu la kuchangia.
Mhe. Anamringi Macha amewaeleza wajasiriamali wa kata za Bugarama na Bulyanhulu kuwa Serikali ya awamu ya tano kwa kutambua jitihada zinazofanywa na wajasiliamali hao iliona ni vema kuwategenezea vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo ili kuwaondolea usumbufu waliokuwa wakiopata awali kwa ama kupoteza bidhaa zao au kukamatwa na askari hivyo ndugu zangu changamkieni fursa hii. Ili uweze kupata kitambulisho hiki ni lazima uwe na mauzo ghafi yasiyozidi Tsh. Milioni 4 sambamba na kujaza fomu maalum ya utambulisho na kuiwakilisha Halmashauri nami naagiza “ mkurugenzi Mtendaji (W) mtu kama amekidhi vigezo apatiwe kitambulisho chake ndani ya masaa 48” kama hajakidhi vigezo aelezwe wazi wazi.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO
MSALALA
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.