Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania imeupongeza uongozi wa Halmashauri ya Msalala
ukiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Ndg. Simon Berege na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo MHE.
Mibako Mabubu kwa kazi nzuri zinazofanyika katika Halmashauri hiyo. Pongezi hizo zimetolewa
leo tarehe 16/07/2018 na Waziri Mkuu wa Tanzania MHE. Majaliwa Kassim Majaliwa wakati wa ziara
yake ya kikazi ndani ya Halmashauri hiyo.
MHE. Kassim Majaliwa amesema MHE. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli
anatambua kazi nzuri zinazofanywa na wafanyakazi wa Halmashauri ya Msalala na timu nzima ya Baraza
la Madiwani, na ndiyo maana anaunga mkono jitihada hizo kwa kuboresha huduma za Afya katika Halmashauri
hiyo ambapo kwa mwaka 2017/18 Serikali ilitoa Milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya mama na mtoto,
Maabara ya kisasa, jengo la upasuaji, jengo la kuhifadhia maiti na nyumba ya Daktari katika kituo cha
Afya Chela. kazi ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ndg. Simon Berege, watumishi wake na Baraza la
madiwani wameifanya kwa kiwango cha juu cha ubora.
MHE. Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi katika mradi huo ambao tayari umeanza kutumika, MHE. Waziri Mkuu
ameomba Halmashauri iangalie uwezekano wa kupanua eneo la kituo hicho kwani kimepakana na makazi ya wananchi. Serikali
katika mwaka huu 2018/19 imetoa milioni 400 kwa ajili ya ujenzi kama huo uliofanyika lakini awamu hii ujenzi huo
utafanyika katika kata ya Ngaya ambapo zahanati ya Ngaya imepandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya kwani zahanati
hiyo hupokea wagonjwa kutoka kata za Kashishi, Bulige, Mwanase, na maeneo ya Halmashauri jirani za Shinyanga vijijini
na Kahama Mji. Nae Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo Dr. Thom Mtoi amethibitisha kuwa tayari kiasi hicho kimepokelewa
katika akaunti za halmashauri na kwa sasa wapo tayari kuanza utekelezaji wa ujenzi huo.
Mkurugenzi Mtendaji ameishukuru Serikali kwa kuleta fedha kwa wakati na ameahidi kuanza utekelezaji mapema, na kwa upande
wao wananchi wameipongeza Serikali kwa kuwathamini kwani kumekuwa na maboma mengi ndani ya Halmashauri ambayo yanahitaji
Serikali kumalizia ili yaanze kutoa huduma hivyo kuleta pesa na kuipandisha hadhi zahanati ya Ngaya kutasaidia kutatua kero
ya huduma ya Afya kwani wananchi wengi walitegemea kwenda kahama kupata huduma hivyo uwepo wa kituo cha Afya Ngaya kutasaidia
kupunguza gharama za kusafiri.
Imetolew na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Msalala.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.