Kuwepo kwa wawakilishi wa wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala kutoka chama tawala (CCM) yaani kuwepo kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mbunge wa jimbo la Msalala na Wah. Madiwani wote kutoka CCM kumeelezwa kuchangia kukamilika kwa miradi mingi ya kiuchumi kwa kuwa wawakilishi wao huongea lugha moja kwa lengo la kutekeleza ilani ya CCM na ahadi zilizoahidiwa na viongozi hao. Maneno haya yamesemwa na mgeni rasmi Mhe. Benedicto Manowali makamu mwenyekiti wa Halmashauri hiyo wakati wa hafla fupi ya kumkabidhi mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa maji ya ziwa viktoria toka kata ya ngaya hadi kata Busangi.
Nae Mhandisi wa maji wa Wilaya ya Msalala mhandisi Chogero akiutambulisha mradi wa maji kutoka kata ya Ngaya kwenda eneo la makao makuu ya Halmashauri hiyo yaliyopo katika kata ya Ntobo amesema mradi huo utajengwa kwa awamu mbili ambapo katika awamu ya kwanza utayafikia maeneo mengi ya kata ya Busangi na mradi unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 24 sawa na miaka 2. Amemtaja mkandarasi atakayefanya kazi hiyo kuwa ni Kampuni ya Jonta investment company LTD ikishirikiana na kampuni ya Fema Builders iliyopo Shinyanga ambapo mradi utagharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 4.1 ambapo fedha zote zimetolewa na Serikali kuu kwa lengo la kuondoa kero ya maji katika kata za Chela, Busangi na Ntobo.
Akimtambulisha mhandisi wa kandarasi hiyo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala amewataka wananchi wa kata ambapo mradi utapita katika maeneo yao kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na kuwa walinzi wa vifaa vyote vitakavyotumika sambamba na kutoa taarifa pale ambapo wataona mkandarasi haendi sawasawa na matakwa ya mkataba. Dr, Ntanwa Kilagwile amesema fedha za mradi huo zitafanya kazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu ya maji katika maeneo husika sambamba na ulazaji wa mabomba , ununuzi wa mabomba pamoja na ujenzi wa ofisi moja.
Nae Diwani wa kata ya Busangi mhe. Mihayo amewataka wananchi kuchangamkia fursa kwani katika mradi huo watahitajika vibarua na chakula hivyo kumwomba mkandarasi kuajili vibarua wa maeneo husika ili waweze kujiongezea kipato. Mhe. Mihayo ameendelea kutoa shukrani zake kwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Pombe Joseph Magufuli kwa kutekeleza vizuri ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa vitendo na hivyo kuwaomba wananchi wa kata ya Busangi kumuunga mkono Mhe. Rais kwa kutoa maeneo yao bure ambapo mradi utapita sambamba na kuwa walinzi wa mradi huo.
Imetolewa na Kitengo cha Teknolojia Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.