Viongozi wa Kata na Vijiji ndani ya Halmashauri ya Msalala leo wameaswa kuhakikisha wanasimamia zoezi la ukusanyaji mapato
ndani ya maeneo yao ya Utawala na kuhakikisha vyanzo vyote vinakusanywa na fedha kuwasilishwa Serikalini ili wananchi
kupitia Serikali wawezeshwe kutatuliwa kwa changamoto zinazowakabili kama Maji,Umeme,barabara,elimu na afya kwani vitu
vyote hivyo vinahitaji raslimali fedha hivyo mapato yakisimamiwa ipasavyo fedha zitapatikana na kutatua kero za wananchi.
Ujumbe huu umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji(W) Ndg.Khamis Katimba wakati akifungua mafunzo ya mfumo wa usimamizi na matumizi
ya fedha (FFARS) zinazoletwa na Serikali kuu katani na vijijini kwa ajili ya kukamilisha miradi mbalimbali ngazi ya vijiji
kwani Serikali inapeleka fedha moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma kama hospitalini,mashuleni,ofisi za kata na vijiji.
Halmashauri imeona ni vema watendaji wa kata na vijiji wapewe mafunzo ili kurahisisha usimamizi wa fedha zinazotolewa.
Kwa upande wao viongozi wa kata na vijiji wamempongeza Mkurugenzi Mtendaji(W) huyo kwa kuwajali kwani tangu afike ndani ya Halmashauri
amewatembelea katika maeneo yao ya kazi na kutatua changamoto mbalimbali sambamba na kuwaita Halmashauri kwa ajili ya kuwajengea uwezo
hasa katika zoezi zima la usimamizi wa mapato kwani ndiyo kipaumbele cha kwanza cha kiongozi huyo na kuahidi kutomwangusha kwani mafunzo
haya yatawasaidia kuhakikisha haki inatendeka na mapato kukusanywa ili jamii iweze kufaidika na matunda ya Serikali yao tukufu inayoongozwa
na Rais Samia Suluhu.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.