Wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga watakiwa kuchangamkia fursa za uwekezaji zinazotolewa nchini.
Rai hiyo imetolewa na waziri wa nishati mh. Dk. Medard Kalemani wakati akizungumza na wananchi wilayani Kahama mkoani Shinyanga wakati wa kikao kazi cha viongozi wa serikali, wafanyabiashara, viongozi wa mashirika ya kidini na binafsi mwanzoni mwa wiki hii.
Mh.Dk Kalemani amesema kuwa bomba hilo lenye urefu wa km 1445 litapita katika mikoa nane ya Tanzania ambayo ni mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Singida, Tabora, Dodoma, Manyara, Arusha na Tanga na katika wilaya 24 ikiwemo wilaya ya Kahama ambapo kitajengwa kituo kikubwa cha usanifu wa mafuta katika kata ya Isaka na hivyo hii ni fursa kwa wana Msalala, Kahama na Shinyanga kwani itatoa ajira kwa Watanzania kwa kuwa zaidi ya asilimia 80% ya mradi huo utakuwa nchini Tanzania
“Mradi huu ni fursa kubwa kwetu sisi kama Watanzania kibiashara na ajira na tunatarajia utatoa ajira zaidi ya elfu kumi wakati wa ujenzi na baada ya ujenzi ajira za muda mrefu wa kati na za muda mfupi pia zitatolewa’’dk Kalemani amesema.
Aidha Mh.Dk Kalemani amewataka wananchi wilayani Kahama kuupokea mradi huo kwa mikono miwili na kutoa ushirikiano kwa serikali ili mradi uweze kutekelezeka kirahisi,na kwamba ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi mei mwaka huu wa 2018 na kukamilika mwaka 2020.
Akifafanua maswala ya fidia waziri wa nishati amesema kuwa serikali inafanya juhudi za kuhakikisha watanzania wanapata fursa kwanza na kutumia sera na sheria za Tanzania katika kutoa fidia kwa wananchi ambao ardhi zao zitatumika katika ujenzi wa bomba hilo la mafuta ili kuwalinda na kuhakikisha wanapata fidia zao stahiki. Aliongeza kwa kuwataka washiriki wote wa kikao kazi hiki kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa wananchi watakuwa na uelewa wa kutosha juu ya suala hilo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Halmashauri ya Msalala.
Haki Miliki ©2017 Halmashauri ya Msalala. Haki zote zimehifadhiwa.